Na Matereka Jalilu
KAMA ingekuwa mchezo wa soka ni dini basi duniani kungekuwapo na dini moja kubwa ambayo ni mpira wa miguu na sio kwamba michezo mingine haina wapenzi la hasha! Bali ni kutokana na ukweli kwamba mpira wa miguu kwa sasa ndio unafuatiliwa na watu wengi zaidi duniani kuanzia watoto, vijana na wazee, siku hizi wanawake nao wameingia kwa wingi kwenye kuufuatilia mchezo huu tofauti na miaka ya nyuma, hii ni nje na wale ambao hawakuwa na uelewa wowote juu ya mchezo huo lakini wameendelea kuufuatilia kupitia michezo ya kubashiri (Betting) sehemu mbalimbali duniani.
Ukiachana na dunia kuupenda mchezo huu, ngoja nikueleze kidogo kuhusiana na ushabiki wa soka nchini kwetu ‘bongo’ neno ambalo linatumika kuitambulisha nchi yetu Tanzania kuhusiana na mapenzi yao ya mchezo wa soka ilivyo na maajabu yake ambapo licha ya ukweli kuwa kuna idadi ya timu nyingi nchini katika kila mkoa lakini imeshindwa kuzuia matabaka makubwa mawili ya timu kuu pinzani tangu enzi.
Ndio, mapenzi ya mchezo wa soka nchini yamebaki kwenye timu mbili za Simba na Yanga pekee na imekuwa kama ilivyo tabia ya kurithi kwani watanzania walio wengi kama sio Simba basi ni Yanga.
Ni ajabu na kweli kwamba licha ya watanzania wengi kuzipenda timu hizo lakini pia hata viongozi wa timu zingine pinzani ya timu hizi mbili ambazo zinapambana nazo kwenye mechi mbalimbali baina yao huwa nao ni ‘wanazi’ wakubwa kwa timu za Simba ama Yanga!
Kama utaondoa dini kuu mbili nchini ambazo ni Uislamu na Ukristo basi kitu kingine chenye wafuasi wengi ni timu hizi mbili za Simba na Yanga ndio maana kila inapokaribia mechi baina yao huwa kuna pilikapilika nyingi kuelekea mchezo husika matokeo yake huwafanya hadi viongozi wa timu hizo kuzipeleka ‘chimbo’ timu zao kwa lengo moja tu kuibuka na ushindi dhidi ya mpinzani.
Sasa timu hizo mbili pinzani zaidi nchini na ukanda wote wa Afrika Mshariki na Kati ukiwa ni mchezo namba 3 kwa upinzani zaidi barani Afrika, zitakutana dimbani Jumamosi hii Oktoba 28 ukiwa ni mchezo wa raundi ya 8 ya ligi kuu bara, ambapo kuelekea mtangane huo makala haya yanakuletea mambo matano ambayo yanaweza kuwa ngao ya ushindi kwa timu mojawapo kulingana na timu zote mbili zilivyo.
Kete 5 muhimu zinazoweza kuamua matokeo
- Uwiano wa pointi
Ukiutafuta msimamo wa ligi kuu bara utaona kwamba timu hizi mbili zimefungana alama sawa zikijikusanyia alama 15 kila moja na kufanana kwenye idadi ya mechi walizoshinda na walizotoa sare jambo ambalo linamaanisha kuwa timu itakayoibuka na ushindi kwenye mtanange huo ndio ina nafasi kubwa ya kuongoza msimamo dhidi ya mwenzake nje na matokeo ya mchezo wa Mtibwa Sugar dhidi ya Singida United Jumapili.
Katika msimamo huo timu zote mbili zimelingana idadi ya alama na tofauti baina yao ni idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa ambapo Simba imefunga mabao 19 na kufungwa bao 4 baada ya kushinda mechi 4 na kutoa sare mechi 3 wakati Yanga imefunga jumla ya mabao 10 na kufungwa bao 3 ikiwa imeshinda mechi 4 na sare 3 kama ilivyo kwa Simba hali inayopelekea ulazima wa timu moja kutaka kuongoza ligi hivyo kuwepo kwa upinzani wa kutosha kutokana na ukweli kwamba hakuna timu kati yao itakayotaka kuharibu mwanzo wake wa kutofungwa tangu ligi ilipoanza.
- Ushindi mnono mechi iliyopita
Kwa wataalamu wa saikolojia wanaelewa nini maana ya kuliendea jambo fulani huku ukiwa sawa kiakili na kifikra tofauti na atakeliendea jambo hilo akiwa hayuko sawa kwenye nyanja hiyo, hivyo basi kuelekea mchezo wa Oktoba 28 baina ya timu hizo mbili kuna mfanano na usawa wa mambo mawili tayari ambayo ni kulingana kwenye msimamo wa alama 15 kila mmoja lakini lingine ambalo ni jema zaidi ni ushindi walioupata kila timu kwenye mechi zilizopita.
Mchezo uliopita Jumamosi Oktoba 21 Simba ikicheza nyumbani uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ilifanikiwa kuifunga Njombe Mji mabao 4-0 yaliyofungwa na Mzamiru Yassin aliyefunga mawili na Emmanuel Okwi pamoja na Laudit Mavugo.
Upande wa Yanga nao wakicheza ugenini mkoani Shinyanga uwanja wa Kambarage waliifunga Stand United bao 4-0 mabao ya Ibrahim Ajib aliyefunga mawili pamoja na Obrey Chirwa na Pius Buswita.
Kutokana na ushindi huo kwa timu hizo ni moja ya jambo muhimu mno kwenye mchezo huu kwani kila timu itaingia uwanjani ikiwa vizuri ikichagizwa na matokeo ya ushindi mnono wa mechi iliyopita.
- Emmanuel Arnold Okwi
Kabla ya kujiuliza sababu ya mshambuliaji huyu kuwa moja ya vitu muhimu vya kutazama kuelekea mchezo wenyewe tafuta msimamo wa wafungaji wanaoongoza kwa kupachika mabao kwenye ligi kuu hadi sasa bila shaka jina la kwanza ni lake Mganda Emmanuel Arnold Okwi ambaye katika mechi 7 alizokwishacheza amefanikiwa kufunga bao 8 ikiwa ni zaidi ya idadi ya mechi alizocheza kwenye ligi tena tofauti na wenzake ni yeye ambaye amefunga bao hizo kwenye mechi 6 tu kati ya 7 ilizocheza timu yake.
Uwepo wa mchezaji huyu ni silaha kubwa ya kuiwezesha timu yake Simba kuibuka na ushindi dhidi ya Yanga kutokana na uwezo wake wa kucheka na nyavu dhidi ya timu pinzani huku pia alishawahi kuifunga timu hiyo huko nyuma kabla ya kuondoka kuzichezea timu za Etoule du Sahel ya Tunisia na Yanga na baadaye aliporejea Msimbazi na kuondoka kwa mara nyingine alipoenda klabu ya Sonderjyske ya Denmark.
- Ibrahim Ajib Migomba
Hisia za mashabiki wa Yanga kwamba wataibuka na ushindi dhidi ya watani wao wa jadi kwenye mchezo huo kwa kiasi kikubwa zinaanzia kwa kiungo huyu mshambuliaji Ibrahim Ajib Migomba, Ajib amekuwa mhimili mkubwa kwa timu hiyo tangu alipotua akitokea kwa wapinzani wao Simba dirisha la kiangazi iliyopita ambapo licha ya kwamba anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji lakini amefanikiwa kufunga mabao muhimu kweli kweli yaliyofanikisha ushindi na pointi muhimu kwa timu yake na hatimaye kulingana pointi na mahasimu wao Simba.
Ajib pia ndiye anayefuata kwa ufungaji kwenye mpangilio wa msimamo wa wafungaji wa ligi kuu nyuma ya Emmanuel Okwi wa Simba ambapo yeye amefanikiwa kufunga mara 5 ikiwa ni pungufu ya bao 3 dhidi ya Okwi, endapo ataendeleza makali yake bila shaka atakuwa sababu ya timu yake Yanga kuibuka na ushindi dhidi ya timu yake ya msimu uliopita.
Hivyo basi kulingana na ubora wa wachezaji hao wawili (Okwi na Ajib) ni sababu mojawapo kubwa baina timu hizi na wanatarajiwa kuwa nguzo katika mambo muhimu yatakayoamua mchezo huo wa aina yake na pengine kuwa na upinzani wa juu zaidi.
- Rekodi ya Omog
Hili ni jambo lingine ambalo linapaswa kutazamwa vya kutosha kwani linaweza kuwa sababu ya matokeo baina ya timu hizi hususan Simba kwenye mchezo huu kwani tangu alipokabidhiwa jukumu la kuinoa Simba, Joseph Marius Omog katika mechi zote 4 alizocheza dhidi ya Yanga hajawahi kufungwa mchezo wowote ule ambapo mechi mbili ni ligi kuu na mechi mbili tofauti na ligi.
Mechi yake ya kwanza Omog ilikuwa Oktoba mwaka jana katika mchezo wa ligi kuu ambapo aliiongoza Simba kupata sare ya bao 1-1 licha ya timu yake kuwa pungufu uwanjani baada ya kiungo Jonas Mkude kupewa kadi nyekundu na baadaye bao la kona ya winga Shizya Kichuya kumuokoa dakika za majeruhi, mchezo uliofuata wa ligi kuu ilikuwa mapema mwaka huu mwezi Februari ambapo aliibuka na ushindi wa bao 2-1 licha ya timu yake kubaki tena pungufu uwanjani baada ya beki Besala Bokungu kutolewa kwa kadi nyekundu.
Mechi nyingine mbili alizocheza bila kufungwa na Yanga ni ule wa nusu fainali ya kombe la Mapinduzi aliposhinda kwa penati 4-3 pamoja na mchezo wa Ngao ya Jamii mwezi Agosti mwaka huu akishinda kwa penati baada ya sare tasa ndani ya dakika 90.
Swali linabaki Omog atafanikiwa kulinda rekodi yake mbele ya Yanga kwa kuibana na kushinda au kutoa sare au atashindwa kulinda na kupokea kichapo cha kwanza tangu aanze kuinoa timu hiyo?
Lakini pia mawazo mengine kuhusiana na Omog kutimuliwa endapo atafungwa mechi hiyo ni karata nyingine ambayo itafanya mchezo uwe mgumu zaidi kwani kocha huyo hatotaka kuweka rehani kibarua chake kupitia mchezo huu, ni jambo la kusubiri.
Kiujumla kuna mambo mengine kadhaa yanayoweza kuamua mchezo huo lakini hizi sababu kuu 5 ni kati ya mambo muhimu yatakayoufanya mchezo kuwa na upinzani zaidi na ambayo yataamua mchezo baina ya mahasimu hawa wawili wakubwa nchini ambao wanatengeneza ‘Kariakoo Derby’ miongoni mwa mechi kubwa 3 za juu barani Afrika baada ya ‘Cairo Derby’ ambayo huzihusisha timu mbili pinzani nchini Misri, Al Ahly na Zamalek pamoja na ile ‘Soweto Derby’ inayohusisha timu za Orlando Pirates dhidi ya Kaizer Chiefs zote za Afrika Kusini.