Na Baraka Mbolembole
KUELEKEA mchezo wa ‘Dar Pacha’ siku ya Jumamosi hii katika uwanja wa Uhuru, Ibrahim Ajib na Emmanuel Okwi wanaonekana kama ‘miungu’ ambao wataamua pambano hilo la kwanza la mahasimu msimu huu.
AJIB
Ajib ‘hakuwahi kuheshimiwa’ wakati alipokuwa lakini kwa mara ya kwanza namuona akienda kufunga kwa mara ya kwanza ‘goli halali’ katika mchezo huo mkubwa zaidi Afrika Mashariki na atafanya hivyo dhidi ya timu iliyomlea, kumkuza na kumtambulisha katika soka la Tanzania kwa misimu mitano iliyopita.
Magoli yake matano ambayo tayari ameshayafunga katika michezo saba akiwa Yanga yamewapagawisha mashabiki kiasi cha kusahau habari za wafungaji wao tegemeo kutoka ng’ambo ya nchi, Mrundi Amis Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma ambao hawatacheza mchezo huo wa ruandi ya nane kutokana na majeraha.
OKWI
Upande wa Simba, Okwi anatazamwa kwa ‘macho makali,’ wakati mashabiki wa timu yake wakitanguliza magoli 8 ya Mganda huyo aliyesajiliwa kwa mara ya tatu msimu huu, wale wa Yanga bado wanaamini ipo kazi na walinzi wao wanapaswa kuwa makini na kiungo mshambulizi wa timu ya Taifa ya Uganda ambaye tayari ameshafunga magoli manne katika mipambano ya mahasimu hao.
Okwi ameifunga Yanga mara tatu na alifanya hivyo mara moja dhidi ya Simba wakati alipokuwa Yanga kwa miezi 6 mwaka 2014.
‘Hat trick’ ya Mganda huyo vs Ruvu Shooting na goli maridadi la mkwaju wa uliokufa dakika ya mwisho ya mchezo Simba 1-1 Mtibwa Sugar FC ni kielelezo tosha kuwa beki ya Yanga inapaswa kuwa na mikakati mizuri, mbinu na uwezo wa kusoma muda ambao Mganda huyo hufanya matukio ya hatari.
AJIB na OKWI SAWA ILA ‘PILATO’ NI HUYU…
Magoli 13 yaliyofungwa na wachezaji hao wawili, viwango vyao kiuchezaji na ushirikiano wanaotoa kwa wachezaji wenzao, wote wanastahili ‘kushika vichwa vya habari’ kuelekea mchezo wa Jumamosi hii, lakini ‘Jicho langu la Tatu’ linaona mbali zaidi na huko namuona ‘pilato’ tofauti anayeweza kuamua matokeo ya mchezo huo-Si mwingine ni kocha wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina.
‘Nililia’ sana uwepo wa Pius Buswita katika kikosi cha Yanga, niliamini huyu alikuwa mchezaji wa mwisho-kiunganishi wa timu kutoka katikati ya uwanja kuelekea eneo la mashambulizi. Baada ya kumtazama Rafael Daud katika michezo mitatu ya mwanzo niligundua mchezaji huyo anahitaji muda ili kucheza vizuri, niliamini Juma Mahadhi ameshindwa kutumia nafasi aliyopewa kwa zaidi ya miezi 6 na ili Yanga iende mbele, nilimuona Buswita kama mtu ambaye ataenda ‘kuiamsha’ timu katika mashambulizi kwa kufanya kazi ambayo hutakiwa na kocha.
Mchezo wake wa kwanza tu, Buswita akaibuka nyota wa mchezo. Kiwango chake katika michezo Kagera Sugar 1-2 Yanga, huku akifunga na kushiriki katika goli moja katika game iliyopita Stand United 0-4 Yanga kimefanya Yanga kurudi haraka katika harakati za ubingwa huku wakiwa sawa kipointi na vinara Simba.
Lwandamina atakuwa na amani zaidi kwa sababu huenda Mzimbabwe, Thaban Kamusoko atakuwa amerejea kikosini baada ya kukosekana katika michezo vs Kagera Sugar na Stand United. Uwepo wa Mcongo, Papy Tshishimbi ambaye anauwezo mkuwa wa kupora mipira na kuanzisha mashambulizi ya haraka, Kamusoko, Pato Ngonyani na Pius Buswita katika kiungo cha watu wanne kutaifanya Yanga kushambulia kwa haraka na kuwa wagumu kupitika kwa sababu Simba wao hucheza mchezo wa pasi fupi fupi za chini ambazo ni rahisi kuzivuruga.
Obrey Chirwa ambaye ametoka kufunga magoli mawili katika michezo miwili iliyopita na Ajib wanaweza kuwa machaguo sahihi ya kuanza katika mfumo wa 4-4-2. Kama, Lwandamina anataka kuwapa mechi nzuri zaidi mashabiki wa timu yake na kuondoa ‘mzimu’ wa mabingwa hao watetezi kutoishinda Simba katika michezo mitatu iliyopita ya michuano tofauti. Kuendelea kuwapanga Chirwa na Ajib katika safu ya washambuliaji wawili kutaipa Yanga magoli, penati na mipira ya faulo ambayo sasa kwao ni muhimu sana kwa sababu wamepata mtu maalum wa kupiga kiufundi mipira hiyo.
Safu yote ya ulinzi ya Simba inapitika na hata golini bado hawana mchezaji wa kuwanyima Yanga magoli kama wata-shuti vizuri. Mbao FC, Stand United, Mtibwa Sugar wote wameonyesha udhaifu wa Aishi Manula katika uongozi wake wa ngome. Huku Mganda, Juuko Murishid na Mzimbabwe, Method Mwanjale wakitarajiwa kucheza pamoja katika beki ya kati, akili binafsi za Chirwa na Ajib zinaweza kuongozwa na pasi za haraka zinazopigwa katika nafasi na kijana Buswita na hili litawapa magoli, faulo au mikwaju ya penalti kwa sababu walinzi hao wa kati wa Simba wanapenda kuchapa viatu huku wakikosa kasi nzuri wanapopitwa na mpinzani.
Upangaji wake wa kikosi na mfumo atakao utumia Lwandamina ndiyo utaamua mechi hii na naona Yanga ikienda kushinda mechi kwa tofauti ya goli mbili na kwenda kileleni. Yanga wana ukuta mzuri ambao umecheza pamoja kwa michezo sita mfululizo kabla ya kubadilishwa kwa sababu za kitimu katika mchezo wa raundi ya saba ambao walishinda 4-0 ugenini.
Licha ya kuruhusu magoli matatu safu ya walinzi, Juma Abdul, Gadiel Michael, Vicent Andrew na Kelvin Yondan inafaa kuwazima Simba kwa aina yoyote vile watakavyokuja. Kuwapanga Pato na Tshishimbi kama viungo walinzi ni jambo ambalo litawapa faida kubwa Yanga. Watashambulia kwa mipira yao mirefu lakini watakuwa na rundo la wachezaji wagumu katikati ya uwanja jambo ambalo huwapa sana taabu wachezaji wa Simba.