Mechi sita za VPL zimeshapigwa, Kagera Sugar ipo mkiani ikiwa na pointi mbili ambazo imezipata katika mechi ambazo wametoka sare bado hawajapata ushindi hadi sasa.
Yameanza kuzungumzwa maneno mengi juu ya kufanya vibaya kwa Kagera Sugar huku kocha Mecky Maxime akiwa anatajwa kuwa sababu ya timu hiyo kufanya vibaya.
Binafsi bado ninaamini Kagera Sugar itanyanyuka na kufanya vizuri chini Maxime licha ya wachache kuanza kubeza uwezo wake.
Mashabiki wa timu hiyo walibeba mabango wakitaka Maxime aondoke Kagera Sugar kufuatia timu yao kufanya vibaya mwanzoni mwa ligi huku wakibamizwa 6-0 na Yanga kwenye uwanja wao wa Kaitaba.
Msimu uliopita vs msimu huu
Mechi za mwanzo wa ligi msimu uliopita, Kagera ilianza vibaya kwa kuchezea vichapo vya mara kwa mara sawa na msimu huu ambapo hadi sasa bado hawajafanya vizuri.
Msimu uliopita Kagera Sugar ilimaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi nyuma ya Yanga na Simba huku wakiwa juu ya Azam ambao walimaliza katika nafasi ya nne. Hapo ni namna gani Maxime amedhihirisha alivyokuwa mpambanaji ndani ya kikosi cha ‘wanankurunkumbi.’
Katika mechi 30 za ligi msimu uliopita Kagera walishinda mechi 15, wakatoka sare katika mechi saba na kupoteza mechi tano.
Hadi sasa timu yake haijashinda katika mechi sita walizocheza msimu huu kibaya zaidi Kagera haifungi magoli mengi, wamefunga magoli mawili tu katika michezo hiyo sita.
Bado naamini Kagera Sugar itanyanyuka
Ligi yetu jinsi ilivyo bado Kagera Sugar ina nafasi ya kufanya vizuri ikiwa chini ya Maxime na kumaliza katika nafasi waliyomaliza msimu uliopita.
Licha ya kutoshinda hata mchezo mmoja, ina pointi mbili ikiwa mkiani mwa ligi, Simba wanaoongoza ligi wana pointi 12 sawa na timu nyingine tatu (Mtibwa Sugar, Yanga na Azam) Simba na Kagera zinatofautishwa na pointi 10.
Ukiachana na Simba, Mtibwa Sugar, Yanga, Azam, Singida United, timu nyingine bado pia hazijafanya vizuri kwa sababu bado mechi nyingi zimekuwa zikitawaliwa na matokeo ya sare.
Timu bado nzuri
Licha ya kuondokewa na mfungaji wao Mbaraka Yusuph Abeid aliyejiunga na Azam, bado hakumaanishi Kagera Sugar imekwisha.
Kikosi cha Maxime ni kizuri na kina weza kukaa sawa, uwepo wa wachezaji wazoefu kama Juma Kaseja, Juma Nyoso, George Kavila, Geoffrey Taita, Ame Ali ‘Zungu’ wakisaidiana na vijana wanahitaji ushindi wa kwanza ili kuendeleza fomu ya ushindi.