Na Baraka Mbolembole
KUSAJILIWA kwa Mohamed Ibrahim na Muzamiru Yassin katika kikosi cha Simba katikati ya mwaka 2016 wakitokea Mtibwa Sugar FC kulianza kupunguza nafasi ya kucheza kwa Said Ndemla katika kiungo cha mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara.
Wakati anapopata nafasi ya kucheza, Ndemla amekuwa akizua maswali mengi kwa mashabiki hata wale wasio wa klabu yake.
Pasi zake timilifu za kwenda mbele, uwezo wa kuusoma mchezo na kuichezesha timu yake, kukaba nafasi, ‘jicho lake’ la kipekee katika upigaji wa pasi za kupenyeza, na uwezo wa kushuti mpira katika mwelekeo sahihi ni mambo ambayo yamekuwa yakiacha ‘viulizo’, kwanini kijana huyu hapati nafasi ya kutosha katika klabu iliyomkuza na kumpandisha katika kikosi cha kwanza msimu wa 2012/13?
TAYARI AMEKOMAA, ANAHITAJI KUPEVUKA KIMCHEZO
Wakati Simba ilipotwaa ubingwa wake wa mwisho wa ligi kuu Mei, 2012 timu hiyo ilikuwa katika mwelekeo mzuri. Katika kikosi cha wakubwa timu ilikuwa na msimu mzuri ambao ulishuhudia timu hiyo ikifika hadi katika hatua ya 16 bora katika Caf Confederation Cup.
Katika kiungo cha timu hiyo kulikuwa na nyota kama marehemu Patrick Mafisango, Mwinyi Kazimoto katika ubora wake, Salum Machaku , Haruna ‘Boban’, na Emmanuel Okwi ‘mtoto’.
Hawa walitengeneza timu imara iliyokuwa na uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, huku ikiwa imara pia katika kuzuia mashambulizi ya timu pinzani. ‘Kutoweka’ duniani kwa Mafisango kulifungua nafasi ya kusajiliwa kikosini kwa mara ya pili Ramadhani Chombo ‘Redondo’ sambamba na Mrisho Ngassa.
Baada ya kusajili vibaya timu na kuambulia aibu katika Kagame Cup, Julai, 2012, uongozi wa Simba haukutaka kufanya usajili mkubwa tena baada ya kuwatema Wacongoman, Linno Musombo, Kanu na Danny Mrwanda kwa kuamini vipaji vichanga ambavyo vilitarajiwa kupandishwa timu A kutoka katika kikosi chao cha pili Ndemla, Jonas Mkude, Hassan Khatib, Abdallah Seseme, William Lucian na Edward Christopher walitazamwa kama sehemu ya wachezaji muhimu wa kikosi cha timu kubwa hasa baada ya kufanya vizuri katika michuano ya Super 8 na Ujirani Mwema ambayo Simba iliamua kutumia zaidi wachezaji wa kikosi cha pili wakati timu ya kwanza ikiwa katika maandalizi ya msimu mpya wa 2012/13 wakati huo.
Licha ya kwamba hawakupata sana nafasi ya kucheza katika kikosi kilichoanza msimu vibaya chini ya Mserbia, Milovan Circovic, Ndemla na kundi la yosso wenzake waliendelea kujifunza kwa maana hawakuwa wamewahi kucheza ligi yoyote ile ya juu.
Kufanya vibaya mfululizo kwa timu ndani ya uwanja kulipelekea kufutwa kazi kwa Milovan kufikia Novemba, 2012 na Mfaransa, Patrick Liewig akachukua nafasi yake Disemba, 2012.
Liewig aliondoka na sehemu ya timu kuelekea Oman kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili, huku baadhi ya wachezaji wengine wakiungana na wale wa kikosi cha pili kucheza michuano ya Mapinduzi Cup-Januari, 2013 huko Zanzibar.
Mkude na Ndemla walitumia vizuri nafasi hiyo ya kucheza Mapinduzi Cup na haraka wakatokea kuaminiwa na kocha Liewig ambaye aliamua kuwatumia vijana zaidi katika michezo isiyopungua 8 ya mzunguko wa pili katika VPL.
Liewig ndiye aliyeamua klabu kuachana na wachezaji kama Haruna Moshi ‘Boban’, Felix Sunzu kwa kile alichodai ni sababu za utovu wa nidhamu. Ndemla alikuwa kati ya kundi la vijana ambalo Liewig aliamua kuwatumia katika mchezo wa mwisho wa kufunga msimu vs Yanga, Mei, 2013 mchezo ambao Simba ilichapwa 2-0.
Kiwango kizuri ambacho alikionyesha kilimfanya kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni kuamua kuendeleza kile alichokianzisha Liewig-kuwaamini wachezaji vijana waliozalishwa na klabu chini ya Selemani Matola.
King alichukua nafasi ya Liewig ambaye alimaliza mkataba wake wa miezi sita Juni, 2013. King aliendelea kuwatumia kina Ndemla huku pia Abdulhalim Humud na Uhuru Suleimani pia wakirejeshwa kikosini msimu wa 2013/14.
King alikuwa kocha wa tatu kwa Ndemla katika kikosi cha timu ya wakubwa, na wengi wanakumbuka namna Ndemla na Luciani walivyoingia uwanjani wakati Simba ikiwa nyuma 3-0 vs mahasimu wao Yanga na kuisaidia kusawazisha na kutengeneza sare ya kupenda 3-3 katika ‘Dar-Pacha’ Oktoba, 2013.
Mambo yalipoanza kwenda ‘mrama’ King na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ wakaondolewa Novemba, 2013. Mcroatia, Zdravko Logarusic akapewa nafasi na kufikia Agosti, 2014 naye akatimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Patrick Phiri. Mzambia huyo (Phiri) aliongoza timu katika michezo isiyozidi 9 tu ya mwanzo wa msimu 2014/15 kisha akatimuliwa kutokana na matokeo mabaya.
Mserbia, Goran akapewa kibarua cha muda na kocha huyo aliamua kuwatumia zaidi wachezaji vijana na hapo ndipo Ndemla alivyoendelea kukomaa kimchezo. Kuondoka kwa Goran mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2014/15 ilikuwa pigo kubwa kwa wachezaji vijana kama Seseme, Ndemla kwani kocha aliyefuata, Muingereza, Dylan Kerr licha ya kupendelea kuwapa nafasi vijana ila hakuungwa mkono na viongozi naye akaondolewa kufikia Disemba, 2016.
Mganda, Jackson Mayanja akapewa nafasi ya kuwa kocha wa muda na Ndemla aliendelea kubaki mchezaji asiye na nafasi ya kudumu kikosini. Omog ni kocha wa nane ndani ya misimu mitano ambayo Ndemla amekuwa ndani ya kikosi cha Simba na mabadiliko haya ya makocha yanaweza kuwa yamemkomaza kifikra mchezaji huyo kwa maana kila kocha aliyefanya naye kazi alimuachia funzo.
Lakini mabadiliko hayo hayawezi kumfanya kupevuka kimpira kwa maana kila kocha humuweka kando na inapotokea nafasi yake ya kucheza basi ni pale tu inapobidi.
AONDOKE SIMBA SASA
Wakati, Christopher, Seseme na Miraj Adam walipoathiriwa na majeraha na kupelekea kuondoka kwao Simba, vijana wengine kama Miraj Athumani, Khatib, Luciani waliondoka ili kwenda kujaribu sehemu nyingine.
Wengi walijiunga na Toto Africans ya Mwanza msimu wa 2014/15 na huko walionyesha viwango ambavyo vimewapeleka katika klabu nyingine za juu kiasi. Mkude ameshapata sana nafasi ya kucheza na kufikia hatua ya kuminiwa hadi kupewa kitambaa cha unahodha.
Hassan Isihaka alishakuwa nahodha pia wa kikosi cha Simba msimu wa 2014/15, huku Ibrahim Ajib akitumia vizuri nafasi finyu aliyopata katika safu ya mashambulizi kutangaza kipaji chake na sasa ni kati ya wachezaji wazuri katika soka la Tanzania akiwa na kikosi cha Yanga.
Kundi karibia lote la vijana ambao walitarajiwa kufanya vizuri klabuni Simba kuanzia mwaka 2012 limeshasambaratika, na kufikia sasa 2017 hakuna mchezaji yoyote wa kikosi kile kilichoshinda Super8 aliye na nafasi katika kikosi cha kwanza, huku Mkude na Ndemla tu wakisalia.
Inawezekana wengi wa vijana wale hawajawa machoni na midomoni mwa wapenzi wa soka kulinganisha na wakati wakiwa Simba lakini, Miraj, Isihaka, Khatib, Luciani, Seseme, Ajib, wanaendelea kufanya vizuri katika vilabu vingine.
Ndemla hajawahi kufikia uwezo wake wa juu kiuchezaji na ili afanye hivyo anapaswa kupata nafasi ya kucheza mfululizo walau michezo nane ya ligi. Hawezi kupata nafasi hiyo katika timu ambayo imembadilishia makocha wanane katika uwepo wake Simba.
Anaweza kujituma zaidi na zaidi katika viwanja vya mazoezi lakini bado sajili za watu binafsi katika timu zimekuwa zikimuondoa katika fikra za watawala, na bahati mbaya makocha wenyewe huwa ‘hawana meno’ kwani wengi hulazimika kuwatumia wachezaji wanaosajiliwa kila msimu kwa hofu ya kuwakera waajiri wao.
Mo Ibra na Muzamiru walimfunika sana Ndemla msimu uliopita lakini bado alionyesha umuhimu wake klabuni Simba katika kila nafasi aliyopewa.
Kusajiliwa kwa Mghana, James Kotei wakati wa dirisha dogo Mwezi Disemba, 2016 kulionyesha wazi ni lengo la kumuondoa Mkude katika kikosi cha kwanza kwa sababu mchezaji huyo alionekana msumbufu wakati wa kuongeza kwake mkataba. Lakini ongezeko la Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na uwepo wa Mo Ibra, Muzamiru, Shiza Kichuya, Okwi, Kotei, na Mkude kunafunga kabisa tumaini ya Taifa Stars kumuona kiungo mahiri katika pasi za kupenyeza nchini akiisaidia timu hiyo ya Taifa.
Kumekuwa na ‘ndoto za alinacha’ kuwa Ndemla anakaribia kujiunga na klabu fulani huko Sweden. Siamini kama atanunuliwa wakati hapati nafasi ya kucheza katika timu yake ya sasa. Aondoke Simba, naamini Yanga, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar FC, Singida United na Azam FC ni sehemu sahihi ambazo zitamng’arisha zaidi Ndemla kama ataamua kujaribu changamoto mpya.