Kiungo wa zamani wa vilabu vya Simba, Yanga na timu ya Taifa, Athumani Idd “Chuji” aliwahi kusema kwenye kipindi cha Sports Xtra cha Clouds Fm kuwa alishangazwa walipoenda kucheza mechi za klabu bingwa Afrika nchini Misri, kuanzia Rais mpaka meneja wa vifaa vya michezo klabuni hapo ni wachezaji wao wa zamani.
Kwa Chuji ilikuwa sahihi kushangaa kwa sababu ni nadra kuona hili barani Afrika. Lakini pengine yanayoendelea kutokea inaweza kuendelea kuwa elimu kwa akina Chuji wengine waliokuwepo ambao hawafahamu katika utaalamu wa kielimu baada ya soka.
Mchezaji na golikipa wa zamani wa vilabu vya Ajax, Manchester United, na timu ya taifa ya Uholanzi, Edwin Van Der Sar atakuwa mmoja kati ya wazungumzaji wa mkutano mkubwa wa masuala ya soka maarufu kama Soccerex Global Convention.
Mkutano utakaofanyika 4-6 Septemba, katika jiji la Manchester. Van Der Sar atakuwa sehemu ya ujumbe wa wazungumzaji wakuu ambao ni watendaji wakubwa wa vilabu wakijadili umuhimu wa kuwa na taratibu zinazofahamika ndani ya vilabu vya soka; namna ya kuanzisha na kuendeleza taswira ya klabu na vitu gani vinahitajika kuhakikisha haya mambo yanaendelea kusimamiwa na kuendelezwa.
Akiwa kwa sasa huyu ni mkurugenzi mtendaji wa klabu anayoipenda siku zote ya Ajax, Edwin ameweka machoni kwetu uwezo wake mkubwa kwa zaidi ya miaka 21, akishinda mataji na vilabu mbalimbali ikiwemo Juventus, Ajax na Manchester United. Lakini pia ni huyu ambaye amechezea timu ya taifa mara 13, Van Der Sar anahesabiwa kama moja ya makipa bora wa kizazi chake.
Baada ya kuachana na soka, Van Der Sar alienda kusomea shahada ya uzamili (masters) ya usimamizi/uongozi wa michezo na chapa kwenye taasisi ya Johan Cruyff kabla hajajiunga na Ajax, November 2012 akiwa mkurugenzi wao wa masoko.
Huyu amekuwa sehemu ya timu ambayo imebadili kabisa mfumo na mtinfo wa udhamini kwenye klabu ya Ajax na kukuza mwenendo wa chapa ya klabu hiyo duniani kote, na kusambaa kwenye masoko mengi kama bara la Asia. Kwa sasa akiwa kama mkurugenzi mtendaji wa klabu, Van Der Sar ni sehemu ya kundi la wachezaji bora waliochukua nafasi kwenye klabu hiyo pamoja na Dennis Bergkamp na Marc Overmars tangu waamue kustaafu.
Kwenye mkutano huo mkubwa wa kidunia, Edwin atatumia uzoefu wake mkubwa ndani na nje ya uwnaja kutoa elimu kubwa yenye thamani na muhimu kwenye ugeni utakaokuwepo. Kazi kubwa aliyoifanya kwa miaka ya karibuni akiwa na Ajax imeegemea zaidi kwenye chapa ya klabu hiyo.
Lakini pia akihakikisha anatoa sifa na kusambaza sifa za filosofia ya klabu hiyo duniani.Ajax imekkuwa sehemu ambayo inasifika kwa ubora wa kufundisha mbinu bora, kukuza vipaji na Edwin atafundisha namna haya yanavyofanikiwa.
Hili ni jambo moja la msingi ambalo ni nadra kwa wwachezaji wetu wa ndani, jambo halipatikani na ambalo halijawahi kutiliwa mkazo. Ni aibu kuona kuwa sehemu kubwa ya uongozi wa soka letu upo chini ya watu ambao hawakuwahi kuwa wachezaji, kuanzia makocha, viongozi wa klabu mpaka timu ya taifa.
Lakini bahati mbaya ni kuwa wachezaji nao wamebweteka hakuna anayehitaji kuwa Van De Sar mpya au Giorgio Chiellin ambaye majuzi tu ametoa kuchukua shahada ya Uzamili huko Turin akifanya utafiti wa chapa na masoko ya Juventus. Aibu iliyoje, lakini inatakiwa tujifunze kutoka kwenye aibu hii.
Wachezaji wetu wa zamani wanatakiwa wakaongeze elimu, wasimamie vilabu hivi. Elimu zinazohusisha masoko na michezo, uongozi na michezo zipo nyingi na inaweza kusaidia kuondoa vilio vya kila siku vya soka letu kukosa watendaji sahihi.
Leo tungekuwa na akina Aly Mayay, Pawasa, Sekilojo Chambua wanaoongoza soka letu vyema. Bahati mbaya kupanga ni kuchagua. Alichopanga Van De Sar, Girogio Chiellin sicho walichoamua kuchagua akina Mayay na Pawasa wetu.