Barcelona wanahitaji historia nyingine leo usiku ili kuendelea kubaki katika michuano ya ulaya – ni ngumu lakini kuna sababu za kuamini kwamba kikosi cha Luis Enrique kinaweza kufanya maajabu tena msimu huu.
“Tuna asilimia 1 ya kufuzu, 99% zipo pande zote, tukiwa na imani na kuomba Mungu, magoli yatakuja tu.” – alisema Neymar ambaye aliiongoxa Barcelona kugeuza matokeo dhidi ya PSG na sasa anasisitiza kuna uwezekano wa kufanya hivyo tena. Barca wamekuwa na uwezo wa kubadili matokeo lakini pia wamekuwa wakipokea vichapo vikubwa.
Pamoja na ushindi wa 3-0 jijini Turin wiki iliyopita, Juventus wana kumbukumbu ya ushindi wa Barca dhidi ya PsG vichwani mwao. “Barca ni kama Papa baharini, pindi tu wanaponusa damu.” Alisema Giorgio Chiellini ambaye pia amesisitiza haiwezekani kuondoa uwezekano wa Barca kugeuza matokeo. Sasa tuangalie sababu zinazotajwa kwanini Barca wanaweza kugeuza tena matokeo.
Messi
Watu walio karibu na Messi wanasema amepania kubadilisha matokeo na kuisaidia timu yake kufuzu nusu fainali. Kama alivyoonekana kwenye mchezo dhidi ya Real Sociedad, moyo wake wote upo katika mchezo wa usiku wa leo.
Katika La Liga tayari ameshafunga magoli 29 na anaongoza kwa ufungaji katika ligi ya mabingwa wa ulaya akiwa na magoli 11, ana upungufu wa magoli 11 tu kutimiza idadi ya magoli 500 akiwa na Barcelona. Kama Barcelona watataka kutimiza mageuzi mengine ya matokeo katika msimu huu basi watahitaji Muargentina huyu kuwa katika kiwango chake bora kabisa – na akiwa kwenye kiwango chake cha juu hakuna wa kumzuia.
Sergio Busquets IS BACK
Bila uwepo wake, Barca walikuwa dhaifu jijini Turin, asipokuwepo dimbani timu inakosa kiungo muhimu katikati. Safari hii atakuwa na uwezo wa kumuweka Dyabala kwenye ulinzi na kuipanga vizuri timu ambayo safu yake ya ulinzi imeruhusu magoli 7 katika mechi za hivi karibuni. Busquets anajua vyema namna ya kuilinda safu yake ya ulinzi tofauti na Mascherano aliyecheza katikati wiki iliyopita.
The Blaugrana watahitaji kutoruhusu goli na kuwahi kufunga la mapema ili kuweza kuiongezea Juve presha na kupata magoli mengine na ili kufanya hivi wanahitaji mtu aina ya Busquets anakuwa kiungo muhimu kati ya safu ya ulinzi na ushambuliaji.
Mbinu za kiufundi
Je tutaona mfumo wa 3-4-3 au mwingine au tuliozoea wa 4-3-3? Barça wanaweza kuwashtua Juve na mfumo wa uchezaji watakaouchagua. Kule Turin, waitaliano walitumia udhaifu wa mbinu ya Enrique kupanga mabeki watatu nyuma wakimtumia mchezaji kama Cuadrado.
Jordi Alba anaweza kurejea kikosini, huyu anaweza sana kuleta matatizo akishirikiana na Neymar – hili litampa shida sana Dani Alves. Sergi Roberto, pia kama ilivyokuwa katika mchezo vs Real Sociedad, anaweza kuwa na mchango mkubwa katika mfumo wa 4-3-3.
Kumbukumbu za nyuma
Kwa mara 3 Barcelona wamewahi kufanikiwa kubadilisha matokeo ya magoli 3-0 katika mashijdano ya UEFA. Mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 1977-78 dhidi ya Ipswich Town ambapo walipoteza mchezo wa kwanza wakaenda Camp Nou kushinda kwa penati. Mara ya pili ilikuwa msimu wa 1978-79 vs Anderlecht hapa pia walisawazisha na kisha wakaenda kushinda kwa penati. Halafu ukaja mchezo mwingine ambapo walitanguliwa 3-0 na Gothernberg kisha wakaenda kushinda mchezo uliofuatia msimu wa 1985-86 kwa penati tena.
Halafu kuna huu mchezo wa majumaa kadhaa yaliyopita vs PSG ambapo walitanguliwa 4-0, kolichotokea Nou Camp ni historia…….
Machinjoni Camp Nou
Kama kuna sehemu ambayo Barca wanaweza kukufanyia unyama wa kisoka basi ni Camp Nou – ushahidi pekee ni takwimu za msimu huu tu katika mechi za ulaya zilizopigwa katika dimba hili msimu huu: Matokeo yote waliyopata Bsrcelona dhidi ya timu zote walizocheza nazo katika Champions League msimu huu yangetosha kabisha kuwaondoa Juventus katika michuano, Celtic alikufa 7, Monchengladbach alipigwa 4 na Guardiola na City nao walikula 4, PSG akapigwa 6, leo waitaliano watagongwa ngapi?