Na Baraka Mbolembole
Mawenzi Market inakaribia kupanda daraja-kutoka ligi daraja la Pili hadi ligi daraja la kwanza Tanzania Bara msimu ujao. Polisi Moro FC inaweza kurejea ligi kuu kwa mara ya nne kama itafanikiwa kupata matokeo katika michezo yao miwili iliyosalia katika ligi daraja la kwanza 2016/17.
Mwaka mmoja uliopita, timu ya Burkina Faso FC iliteremka daraja kutoka ligi daraja la kwanza hadi ligi daraja la Pili. Sabasaba United ina uhakika wa kubaki ligi daraja la pili msimu ujao. Hizi ni timu nne ambazo zinapatikana katika Manispaa ya Morogoro.
Timu hizo zotezipo madaraja la ya chini (daraja la pili na lile la kwanza.) Kwa mkoa ambao umetoa wachezaji wengi waliotamba/wanaotamba katika soka la Tanzania hivi sasa ni aibu kuona hakuna timu ya ligi kuu inayotoka mjini zaidi ya Mtibwa Sugar FC ambao wanatokea Turiani-nje ya mji wa Morogoro.
NINI TATIZO LA SOKA LA MOROGORO?
Mwaka 2003 nilihamia Morogoro na mwaka mmoja baadae nilikuwa sehemu ya timu ya Mkoa U17 ambayo ilishiriki michuano ya ‘kusaka vipaji’ iliyoandaliwa na raia wa Denmark na kuratibiwa na Shule ya Sekondari Makongo mwaka 2004.
Nakumbuka wakati wa mchakato wa kupata vijana 14 ambao walipaswa kusafiri kuja Dar es Salaam kushiriki michuano ile, kuna watu walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha timu bora ya Mkoa wa Morogoro inapatikana.
Rajab Kindagule, Kocha Maulid ‘Ticha Mau’, marehemu Yahya Berlin na Allan Sigo hawa ni watu muhimu sana katika soka la Morogoro. Walijitolea bila malipo kuwasimamia vijana wengi wenye vipaji na kuwaendeleza kimpira. Hawa ndiyo waanzilishi wa Moro Youth ‘Moro Kids’
Pengine bila watu hao leo hii Tanzania isingekuwa na Juma Abdul, Gideon Sepo, Ayoub Kitala, Hassan Kessy, Salim Mbonde, Willium Lucian, Shomari Kapombe, Kelvin Sabato, Zubery Daby, Miraj Adam, Elias Wironja, Muzamiru Yassin, Shizza Kichuya na wengineo ambao wanatamba katika klabu za ligi kuu Tanzania Bara hivi sasa.
Nakumbuka miaka ya 2000 hadi 2007 Mkoa wa Morogoro ulikuwa na timu takribani tatu hadi nne zilizokuwa zikicheza ligi kuu ya Tanzania Bara. Mtibwa Sugar ambayo haijawahi kuteremka daraja tangu walipofanikiwa kupanda mwaka 1997, Reli FC ‘kiboko ya vigogo’ iliyoteremka daraja mwaka 2002 kisha ‘kufa’ kabisa.
Polisi Moro FC ambayo ilipanda ligi kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2002 na Moro United ambayo ilikaribia kutwaa ubingwa wa VPL mwaka 2005 na ule wa Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati-Kagame Cup 2006. Kwanini sasa imebaki Mtibwa Sugar pekee katika VPL?
1: UBINAFSI
Miaka zaidi ya nane niliyopata kuishi Morogoro niligundua katika soka la Mkoa huo, ubinafsi umetawala kwa kiasi kikubwa licha ya kwamba kuna watu kama Kindagule, Ticha Mau, Allan Sigo, Mkufunzi John Simkoko, Amri Ibrahim, Jimmy Lengwe na wengineo ambao wanajaribu kuufanya mpira wa miguu mkoani humo kuwa na uhai.
Ubinafsi naouzungumzia mimi ni ule wa makocha wakubwa katika soka la Morogoro kuwachukia baadhi ya wachezaji wenye vipaji kwa sababu zisizo za kimpira. Upande wangu naamini kila ‘mwanasoka ni mtoto’ hivyo kuna wakati anaweza kukosea.
Makocha wengi wa mkoa wa Morogoro wanapenda ‘kuabudiwa’ na inapotokea mchezaji mzaliwa wa pale kupishana nae lugha atamtengenezea ‘vizingiti vingi’ na kuhakikisha mchezaji husika hapati nafasi ya kuendelea kucheza katika timu zenye mwelekeo.
Ukifuatilia historia za wachezaji kama Juma Liuzio, Edward Christopher (hawa ni baadhi tu) utagundua kuwa ndani ya Manispaa ya Morogoro ni kugumu sana kwa mchezaji/mzaliwa au kijana wa muda mrefu. Ili uwe mchezaji wa ligi kuu ni lazima uondoke Morogoro mjini ‘kimyakimya’ na kutafuta mahala kwingine kwa kuendeleza ndoto zako.
Wakati ule Reli FC ikiwa chini ya mkufunzi, Dr. Mshindo Msolla timu hiyo ilikuwa ikiwatumia zaidi wachezaji wenyeji wa Morogoro ndiyo maana Reli ilikuwa ‘timu pendwa sana’ na wakazi wa Morogoro na hadi wakati huu timu hiyo ina mashabiki wake wengi licha ya kwamba ‘ipo kuzimu’ kwa
miaka 14 sasa.
Polisi Moro FC imeshindwa kupata mashabiki wa kweli katika Manispaa kwa sababu timu hiyo ya Jeshi la Polisi Morogoro imekosa shukrani. Kila inaposhuka daraja vijana wa Morogoro na kocha John Tamba wamekuwa wakipewa nafasi na wanapofanikiwa kuipandisha timu katika ligi kuu wote ‘wanatupwa’ huku uzoefu ukichukuliwa kama ‘fagio’ la kuwaondoa katika timu.
Mara nyingi Polisi Moro imekuwa ikiteremka daraja chini ya makocha wanaokabidhiwa timu baada ya kupanda ambao nao huwasajili wachezaji wanaowataka na kuwaacha wale waliopigania kuhakikisha timu inapanda.
Mwaka 2004 nilipata bahati ya kufanya majaribio na kushiriki katika kila kitu kama mchezaji wa Polisi Moro kwa zaidi ya mwezi mmoja, nilichong’amua ni kwamba ndani ya safu ya uongozi wa timu hiyo wakati huo ndiyo kulijaa matatizo, chuki, majungu na upendeleo. Sijui sasa hali ikoje lakini miaka miwili iliyopita wakati timu hiyo ilipoteremka daraja kwa mara ya nne mambo yalikuwa vilevile.
2: MASHABIKI MORO WANAPENDA MPIRA, HAWAZIPENDI TIMU…
Si tu Polisi Moro FC, Mtibwa, na hata Moro United ni timu ambazo hazijawahi kupata mashabiki wengi ndani ya Manispaa ya Morogoro na sababu kubwa ni timu hizo kutowapa nafasi ya kutosha wachezaji wazawa wa Morogoro.
Kama unakumbuka wakati Mtibwa inatwaa mataji mawili mfululizo ya VPL miaka ya 1999 na 2000 mkufunzi, Simkoko aliwapa sana nafasi wachezaji wenye vipaji kutoka mkoani humo lakini baadae hali hiyo ikaondoka na Mtibwa ikawa inasajili sana wachezaji kutoka nje ya Morogoro na kuviacha vipaji vingi vya Morogoro vikiangamia mitaani.
Jambo hilo ndio lililosababisha timu hiyo kuukimbia uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa sababu walikuwa wakizomewa katika michezo yao na mashabiki wachache waliokuwa wakiingia uwanjani kutazama mechi zao. Kuanzia mwaka 2008 Mtibwa ilianzisha utaratibu wa kuwachukua vijana wa Morogoro na kuendeleza vipaji vyao na hilo kiasi linawapa mashabiki. Moro United ilitumia pesa nyingia 2004-05 lakini si vijana wa Morogoro waliopata kunufaika na uwekezaji uliofanywa na tajiri/mmiliki wa zamani wa timu hiyo, M. Balhabou hilo liliwachukiza wadau wengi wa mpira mkoani humo na hivyo hawakuwa karibu na klabu hiyo.
Watu wa Morogoro wanapenda sana mpira na ukitaka kuamini hilo nenda mida ya jioni katika viwanja mbalimbali pale Manispaa na utajionea mwenyewe namnamashabiki wanavyofuatilia mazoezi tu ya timu zao za mitaani.
Kuna wakati MDFA Chama cha Soka Manispaa kiliweka utaratibu wa kuzuia mechi yoyote kuchezwa katika ligi za mitaani ikiwa Jamhuri kuna mechi ya ligi kuu, yote ni kwa sababu mashabiki walikuwa wakijazana kutazama vipaji na mpira mzuri unaochezwa mitaani na vijana wa Morogoro kuliko kwenda Jamhuri kutazama mechi ya Simba na Mtibwa.
3: DHARAU
Mwaka 2004 mwalimu Allan Sigo alinifanyia mpango wa kujiunga na Sekondari ya Makongo na kila kitu kilienda sawa. Nilikuwa na miaka 18 wakati huo lakini sikuwa tayari kwenda Makongo kwa kuamini tayari nilikuwa nimekomaa kucheza soka la ushindani. Sigo,hakuchoka alipoona nimegoma kwenda Makongo akanipeleka Burkina Faso ambayo ilikuwa ligi daraja la pili wakati huo.
Nilienda Burkina lakini baada ya mwezi mmoja niliamua kujiondoa katika timu kwa sababu sikupenda kufundishwa na kocha Mzee Mzigila ambaye miezi michache nyuma nilimjibu ‘vibaya’ baada ya kunitusi’ mazoezini wakati naichezea Uruguay FC. Vijana wengi hatukupenda kudharauliwa na wengi tulichukulia vipaji vyetu kama sababu ya kufanya vile tulivyotaka.
Niwe mkweli, wakati mwingine makocha wanakuwa sahihi katika maamuzi yao na ni ngumu sana kwa wachezaji vijana wa Morogoro kuwa watiifu kwa sababu wengi wanaamini vipaji vyao ndiyo kila kitu.
Kushuka kwa mpira wa Morogoro licha ya uwepo wa vipaji vingi katika ligi ya Tanzania Bara kunasababishwa pia na tabia mbaya waliyonayo vijana wa mkoa huo.
Wengi ni wavivu wa kufanya mazoezi, hawapendi kukosolewa, na wana dharau kwa makocha wao. Mwalimu anaweza kusema saa kumi kila mchezaji awe tayari mazoezini lakini wengi wanaweza kuzidisha saa moja zaidi. Hili pia ni tatizo ndiyo maana makocha wasio wavumilivu huwafungia ‘vioo’ vijana wa Morogoro kwa kuamini ni wagumu kuelekezeka licha ya vipaji walivyonavyo.
Mwaka mmoja uliopita kuna kijana nilimpeleka Yanga B kwa kocha Salvatory Edward. Tulifika Kaunda tukiwa tayari tumechelewa kwa dakika 30 na kilichotuchelewesha ni foleni za magari barabarani. Kijana yule nilimuacha akiwa mdogo pale Morogoro lakini niling’amua kipaji chake. Ni mchezaji mzuri sana wa nafasi ya kiungo.
Tulipofika Kaunda nikamwambia, tayari tumechelewa kwa sababu vijana wenzake walikuwa wakiendelea na program za mazoezi ila nikamwambia ajiandae ‘haraka haraka’ wakati mimi naenda kuzungumza na kocha Salvatory na kumuelewesha kuhusu kuchelewa kwetu.
Nikamueleza kocha naye akanielewa ila kurudi pale nilipomuacha kijana yule nikakuta ndiyo kwanza anamaliza kuvaa soksi ya mguu wa kwanza. Mimi sikufanikiwa kwa sababu kuna wakati nilijiamini kupita kiasi kuhusu kipaji changu nikasahau kuhusu muda. Muda ni jambo muhimu sana katika harakati za mtu.
Nilikasirika sana ila sikumonesha wazi wazi, nikamwambia afanye haraka na aanze kukimbia nje ya uwanja hadi pale atakapohitajika. Baada ya dakika tano hivi kocha Salvatory akaniita kwa ajili ya kuzungumza.
“Mbona kijana mwenyewe anaonekana hayupo tayari, amechelewa lakini hata kukimbia peke yake anategea.” Yalikuwa maneno ya kwanza aliyoniambia Salvatory mara baada ya kuniita. Nilitegemea hilo kwa sababu yule kijana alikuwa ‘zaidi ya staa.’
Baadae akapewa nafasi, mimi nikaondoka zangu kuendelea na mambo yangu. Baadaye mchana kocha Salvatory akaniambia anahitaji kukaa na kijana yule walau kwa wiki moja kwa sababu alivutiwa na baadhi ya vitu kutoka kwake. Lakini baada ya sikumbili akalazimisha kurejea Morogoro, sikumzuia nikamuacha aende zake.
Dharau ni sababu nyingine kubwa inayowakwamisha vijana wenye vipaji mkoani Morogoro kwa sababu wanaamini katika vipaji vyao zaidi na sio ‘soka la maadili.’
CHA KUFANYA
Vijana wawe tayari kukosolewa, kuelekezwa, kufanya mazoezi wanayopangiwa. Klabu ziwaheshimu vijana pia na kukubali kuwarekebisha pale wanapoona mapungufu yao. Makocha wapunguze chuki kwa vijana pale wanapokosea, na watawala waheshimu juhudi za makocha wa Morogoro na vipaji vilivyopo.
Mashabiki wazipende timu zao kwa moyo mmoja na kuzisapoti kila zinapokuwa na michezo ya ligi. Umoja ni silaha ambayo itawasimamisha tena Morogoro katika ramani ya soka nchini kama nyakati za kina Profesa Madundo Mtambo.
Utengano haujengi kitu siku zote, jitihada na nidhamu ndiyo siri ya mafanikio. Haya ni machache niliyoyaona mimi katika kuanguka kwa soka la Morogoro licha ya kwamba ndiyo mkoa wenye vipaji vingi bora katika ligi kuu ya Tanzania bara hivi sasa.