Na Baraka Mbolembole
MICHEZO kumi kuelekea mwisho wa msimu wa ligi kuu Tanzania bara 2016/17 mabingwa watetezi Yanga SC wamerejea katika kilele cha msimamo wakiwa na alama 46 baada ya kucheza game 20.
Kikosi cha Mzambia, George Lwandamina na wasaidizi wake Juma Mwambusi na kocha wa makipa Juma Pondamali kitacheza na Stand United siku ya Kesho Ijumaa na ushindi uwafanya watengeneze gepu la pointi nne zaidi dhidi ya wapinzani wao wa karibu Simba SC ambao watacheza na Majimaji FC siku ya Jumamosi katika uwanja wa Majimaji, Songea.
Kuna wakati hata mashabiki wa Yanga walikata tama baada ya timu yao kupoteza 2-1 vs Mbeya City FC mwezi Novemba (kikiwa ni kipigo chao cha pili msimu huu baada ya awali kufungwa 1-0 na Stand United).
Lakini tangu hapo kikosi hicho kimefanikiwa kushinda michezo sita kati ya Saba iliyopita na jambo hilo limerejesha matumaini makubwa kuwa huenda wakafikia malengo yao ya kushinda taji la tatu mfululizo.
Baada ya kufungwa na City Novemba 2 niliandika ili Yanga wafikie malengo yao wanapaswa kuhakikisha hawapotezi mchezo mwingine, pia nilikumbusha kuhusu ‘tabia yao’ ya kutoka chini ya msimamo na kushinda ubingwa inapaswa kurejea. Nakiamini kikosi cha Yanga na ninakichukulia kuwa ni kikosi bora kuliko vyote katika ligi ya Tanzania bara.
Ukiachana na historia yao ya nyuma naamini Yanga ina kila sababu ya kushinda ubingwa wa VPL msimu huu hasa baada ya kuyumba kwa Azam FC. Yanga inabebwa na vitu vingi ambavyo klabu nyingine hazina. Ukiachana na wingi wa mashabiki wao, hizi ni sababu nyingine ambazo ‘Jicho langu la Tatu’ linaona zinaibeba Yanga.
KIKOSI CHENYE WACHEZAJI BORA WAZOEFU NA CHIPUKIZI
Kati ya mambo mazuri ambayo Yanga inanufaika nayo hivi sasa ni kukubali kumuachia mwalimu aliyepita Mholland, Hans van der Pluijm kufanya usajili, hata Lwandamina licha ya kuichukua timu hiyo katika usajili wa mwezi Disemba 2016, viongozi wa Yanga walimpa uhuru na kukubali sajili mbili ambazo alizihitaji ili kuongeza nguvu katika kikosi kilichokuwa chini ya Hans.
Kiungo wa kati, Mzambia, Justine Zulu na yule wa mashambulizi Emmanuel Martin walisajiliwa mwezi Disemba na Lwandamina ili kuongeza hamasa, ubora na upana wa kikosi katika nafasi muhimu. Ukitazama upana wa kikosi cha Yanga hivi sasa unaweza kupata matumaini.
Ally Mustapha,Beno Kakolanya na Deo Dida-hawa ni magolikipa watatu ambao wanaweza kuwa chaguo la kwanza katika vikosi vya timu nyingine. Juma Abdul, Ramadhani Kessy, Oscar Joshua na Mwinyi Hajji ni walinzi wa pembeni ambao yeyote anayepata nafasi ya kucheza hutoa huduma inayotakiwa na benchi la ufundi.
Nahodha,Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Vicent Bossou, Vicent Andrew na Pato Ngonyani ni walinzi watano wenye uwezo mkubwa. Said Juma Makapu, Zulu, Mzimabwe Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima na Juma Mahadhi hawa ni viungo wa kati wenye uwezo wa hali ya juu katika soka la Tanzania.
Deus Kaseke, Geofrey Mwashuiya, Saimon Msuva na Martin ni viungo wanne wa pembeni ambao wote wanaweza kufanya vizuri wakipewa nafasi. Malimi Busungu, Mhilu, Matheo Anthony, Mrundi, Amis Tambwe, Mzimbabwe, Donald Ngoma na Mzambia, Obrey Chirwa ni mastraika sita ambao wanaweza kuisaidia timu kufunga magoli.
Ukitazama kila nafasi katika kikosi hiki ina wachezaji wawili wenye uwezo usiopishana sana hivyo jambo hilo limekuwa likimrahisishia kocha na wasaidizi wake kuwekeza mbinu zao kwa usahihi huku wakiamini hakuna tofauti kubwa anapocheza Mustapha, Beno au Dida, ama Kessy/Abdul.
Kikosi kipana chenye wachezaji bora waliosajiliwa na makocha wa timu kinaibeba Yanga kwa kiasi kikubwa ndiyo maana licha ya kutokuwepo kwa Ngoma bado Chirwa alifanikiwa kuibeba timu katika mchezo mgumu vs Mwadui FC wiki iliyopita.
Jambo muhimu ambalo linapaswa kupewa kipaumbele kwa wachezaji ni kujituma katika viwanja vya mazoezi na kuwa tayari wakati wowote kubeba majukumu ya kuisaidia timu.
NGUVU YA WASHAMBULIAJI
Msuva amekwishafunga magoli 9 katika ligi kuu hadi sasa, idadi sawa na magoli yaliyofungwa na Tambwe. Ngoma na Chirwa wamefunga magoli 7 kila mmoja na Deus Kaseke amekwisha funga magoli 6. Ukijumlisha idadi ya magoli yaliyofungwa na wachezaji hao watano utapa jumla ya magoli 38.
Ikiwa imefanikiwa kufunga magoli 42 katika michezo 20, magoli 38 kufungwa na wachezaji watano ni ishara kwamba mambo yanakwenda vizuri kwa washambuliaji na mchango wao ni mkubwa sana katika mafanikio tarajiwa ya timu yao.
Yanga ndiyo timu iliyofunga magoli mengi msimu uliopita na hadi sasa katika ligi ya msimu huu timu hiyo inaongoza kwa tofauti ya magoli 12 zaidi ya timu inayowafuatia katika ufungaji-Simba SC ambao wamefunga magoli 30.
Ili mafanikio yapatikane ni lazima timu icheze kwa uwiano sawa katika ulinzi, kiungo na mashambulizi na hili limeonekana wazi kwa maana safu ya ulinzi inazuia vizuri ndiyo maana wameruhusu magoli 9 tu.
Viungo wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi ndiyo maana Msuva anaongoza katika upigaji wa pasi za mwisho akiwa ametengenezazaidi ya magoli kumi, Niyonzima na Kaseke pia wamehusika katika magoli zaidi ya kumi yaliyofungwa na wachezaji wengine, huku washambuliaji wakijitahidi kuhakikisha wanafunga magoli ya kutosha kadri itakavyowezekana.
UATAWALA
Achana na matatizo ambayo yaliwahi kuripotiwa kuhusu mishahara ya wachezaji na posho zao kuchelewa mwezi Disemba hali iliyopelekea kuangusha pointi mbili vs African Lyon, achana na sababu za wachezaji kulalamikia mazoezi ya kocha Lwandamina wakati akianza kuifundisha timu hiyo mwezi Disemba, ukweli Yanga wametengeneza timu moja bora sana katika utawala.
Kumuajiri aliyekuwa mchezaji mahiri wa klabu na kocha Charles Boniface Mkwassa katika nafasi ya ukatibu mkuu wa klabu ni jambo jema kwa klabu na hata benchi la ufundi na wachezaji. Uwepo wa Hans kama Mkurugenzi wa Ufundi na makocha Lwandamina, Mwambusi, Pondamali na meneja Hafidh Saleh ni jambo linaloongeza hasama kwa wachezaji.
Watu hawa sita wakishirikiana vizuri na uongozi wa mwenyekiti Yusuph Manji na makamu wake Clement Sanga watazalisha matokeo chaya kwa kiasi kikubwa hadi ndani ya wachezaji.
Umoja, upendo, kuheshimiana na uwajibikaji unatakiwa katika timu hii ya uongozi kisha wao wanapaswa kuwasambazia wachezaji wao pia. Nini kitafuata? Ni mafanikio tu kwa sababu watu wa mpira wamekutana pamoja.
RATIBA
Katika michezo kumi iliyosalia upande wao, Yanga watasafiri mara mbili tu nje ya Dar es Salaam. Wataenda Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar kisha watasafiri kwenda Mwanza kucheza na Mbao FC.
Michezo mingine minane yote watacheza katika uwanja wa Taifa, Dar Es Salaam. Ratiba yao wakiitumia vizuri itawasaidia kushinda ubingwa hasa ukizingatia wapinzani wao wa karibu watakuwa na michezo mingi nje ya Dar.