Na Baraka Mbolembole
MICHUANO ya Caf inataraji kuanza mwezi Februari, 2017. Yanga SC wataiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Azam FC watatuwakilisha katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Timu hizi mbili zimekuwa katika ushiriki wa michuano ya Caf tangu mwaka 2014 na ushiriki wao umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa ‘viporo’ vingi katika ligi kuu Tanzania Bara.
Tuliona msimu uliopita Simba SC ilikuwa mbele kwa michezo minne zaidi ya waliokuwa washindani wao katika mbio za ubingwa-Yanga na Azam FC. Simba iligomea kucheza mechi zake ikitaka Yanga na Azam pia wacheze michezo yao ili walingane.
TFF ilikubaliana na maombi ya Simba na timu hiyo haikucheza hadi Yanga na Azam FC walipocheza na kupunguza michezo yao.
Nimefuatilia ligi za Misri, Zambia, Afrika Kusini na Algeria ambazo bado zinaendelea kuchezwa na kugundua hata katika nchi hizo zinazopiga hatua kimpira na kiuchumi-michezo ya viporo ipo, tena ni mingi zaidi ya ilivyokuwa kwa ligi ya Tanzania Bara msimu uliopita.
Zamalek SC ambayo ilifika fainali katika Caf Champions League msimu uliomalizika Novemba 2016, ilikuwa na michezo zaidi ya saba ya viporo lakini hakuna timu yoyote katika ligi yao iliyogomea kucheza.
Mabingwa wapya wa ligi ya mabingwa-Mamelod Sundowns bado wanaendelea kucheza michezo yao ya ligi kuu Afrika Kusini huku ushiriki wao katika michuano ya Caf ukiwafanya kuwa nyuma ya michezo zaidi ya mitano dhidi ya timu nyingine katika PSL.
Zesco United ya Zambia ambayo ilifika hatua ya nusu fainali katika Caf Champions league 2016, ilikuwa nyuma kwa michezo zaidi ya sita na sasa wanapambana kujaribu kushinda michezo yao ili watetee ubingwa wao.
MO Bejaia ya Algeria ilifika hatua ya makundi katika Confederation Cup 2016, ilikuwa nafasi ya mwisho katika ligi kuu ya Algeria kutokana na kuwa nyuma michezo 7 zaidi ya timu nyingine. Hii ni mifano michache ambayo inathibitisha katika ligi nyingi za Afrika hasa zile zinazokuwa na timu wawakilishi katika michuano ya Caf michezo ya viporo haiepukiki.
Tutarajie michezo ya viporo kwa timu za Yanga, Azam FC na zile ambazo zilipaswa kucheza na wawakilishi hao wa Tanzania Bara katika michuano ya Caf 2017.
Ikiwa Yanga na Azam zitafika katika hatua ya 16 bora-ambayo kuanzia msimu ujao wa Caf hatua hiyo itakuwa ikichezwa kwa mtindo wa makundi ni lazima michezo ya viporo itakuwepo. Hili linapaswa kufahamika sasa ili kupunguza dhana kwamba TFF huwa inazibeba timu fulani.
Ligi kuu za Misri, Afrika Kusini, Zambia na Algeria zote zina idadi ya timu 16 kama ilivyo kwa ligi kuu Bara lakini kutokana na muingiliano wa ratiba ya Caf hata wao wameshindwa kukabiliana na ‘ukosefu wa michezo ya viporo.’ Afrika si Ulaya na inapaswa kueleweka hivyo.