
Chidiebere Abasirim anasema, Novemba 28, 2016 ni siku yake ya furaha zaidi. Hii ni kwasababu siku hiyo aliondolewa waya maalum ambazo alifungwa kwenye kinywa chake kwa ajili ya kushikilia taya zilizovunjika Octoba 12 wakati wa mchezo wa ligi kuu Tanzania bara pale Stand United ikiwa mwenyeji wa Azam FC kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Katika mchezo huo, Chid aliondolewa uwanjani akiwa amebebwa kwenye gari ya wagonjwa na kukimbizwa hospital baada ya kuvunjwa taya na beki wa Azam Agrey Morris. Lilikuwa ni miongoni mwa matukio mabaya kutokea uwanjani kwenye mechi za VPL na liliacha simanzi kwa wachezaji, benchi la ufundi, mashabiki wa Stand pamoja na wadau wa soka nchini.

Baada ya kufanyiwa matibabu, Chidiebere aliambiwa hataweza kula vyakula vigumu wala kuzungumza kwa muda wa wiki sita (6) kutokana na waya alizofungwa kinywani kutoruhusu hayo yote kufanyika ili kuhakikisha anapata nafuu mapema.
Baada ya mshambuliaji huyo kuondolewa waya zote kinywani, nimepata fursa ya kuzungumza nae, anaongea vizuri kitu kinachoashiria amepata nafuu kwa kiasi kikubwa. Nilitaka kufahamu kutoka kwa Chid ni vitu gani ambavyo alivi-miss wakati akiwa amefungwa waya zilizomfanya asizungumze wala kucheza soka kwa muda wote huo huku akila vyakula vyepesi kama uji, juice, kupitia njia maalum.

Chidiebere alikaa bila kuzungumza, wala kufungua kinywa kwa namna yeyote ile kwa muda wa wiki sita (6) na siku tano (mwezi mmoja, wiki mbili na siku tano) lakini sasa hivi anaongea na ameanza kula baadhi ya vyakula ambavyo sio vigumu.
Nili-miss sana kuongea na familia yangu

Waya alizofungwa Chid zimfanya asiongee kabisa kwa muda wote kabla hazijatolewa, hii ilisababisha wakati mgumu kuwasiliana na mkewe pamoja na mtoto wake. Chid anaishi na mkewake Tabitha James pamoja na mtoto wao Chinonso Abasirim.
Njia ambazo jamaa alilazimika kutumia kuwasiliana na mkewe ni ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu pamoja na lugha ya vitendo. Kwa muda wote wa wiki mwezi mmoja, wiki mbili na siku tano, Chid alikuwa akiishi kama bubu ndani ya familia yake.
“Kitu nilichokikosa ni kuwasiliana na familia yangu nili-miss sana kuongea na mke wangu pamoja na mwanagu. Nilikuwa nalazimika kuwasiliana na mama watoto kwa njia ya sms au kwa vitendo, muda wote niliishi kama bubu,” anasema Chidiebere nilipofanya nae mazungumzo kupitia njia ya simu.
Misosi

Chid hakuweza kula vyakula vigumu kwasabau waya alizofungwa hazikuruhusu kufungua kinywa chake kwa namna yoyote ile. Ililazimika atolewe jino moja (gego la chini) ili kupata upenyo ambao atatumia mrija kwa ajili ya kula chakula. Kutokana na hali hiyo, alilazimika kula vyakula vya majimaji vinavyoweza kupita kwenye mrija huo.

Mkewe alilazimika kusaga vyakula ili viweze kupita kwenye mrija. Kwahiyo alikuwa anakunywa uji wa lishe, maziwa, juice, mtori, supu, pamoja na vyakula vingie ambavyo ilimlazimu mkewe kuvisaga na kuwa katika hali ya majimaji au uji.
“Brother nilikumbuka sana misosi. Aina ya chakula nilichokua nakula ilifika wakati nikakumbuka baadhi ya vyakula amvayo sikuweza tena kuvila kutokana na hali yangu niliyokuwa nayo. Ugali, wali, na baadhi ya mboga sikuweza tena kula vitu vidogovidogo vya kutafuna niliishia kuviangalia tu.”
Kuna wakati nilimtembelea akiwa nyumbani kwake Mwanza, mke wa chid aliniambia licha ya jamaa kula kwa mrija lakini alikuwa na uwezo wa kuondosha zaidi ya kilo tatu za misosi kwa siku.
Career ndo kila kitu
Nimekumbuka sana soka, mchezo huu ndio kila kitu kwangu. Kitu ambacho kilikuwa kinanipa mawazo siku za kwanza za majeraha haya ni kama nitaweza kurejea tena uwanjani na kucheza soka. Nijua kila kitu kilikuwa kimemalizika kuhusu maisha yangu ya soka, lakini nashukuru naendelea vizuri siku chache zijazo ntaanza mazoezi baada ya kupata kibali cha daktari.
Tangu Chidiebere alivyoumia, amekosa mechi sita za mwisho za mzunguko wa kwanza wa VPL ambazo hakuna hata mechi moja ambayo timu yake ya Stand United ilipata ushindi.

Michezo sita (6) iliyochezwa na Stand United bila Chidiebere ni pamoja na 15/10/2016 Stand United 1-1 African Lyon, 19/10/16 Tanzania Prisons 2-1 Stand United, 22/10/16 Mtibwa Sugar 3-3 Stand United, 30/10/16 Ruvu Shooting 0-0 Stand United, 02/11/16 Stand United 0-1 Simba na 06/11/16 Ndanda 2-1 Stand United.
Katika kipindi cha majeraha Chid alikuwa akilalamika kichwa kuuma sana hali iliyokuwa inapelekea masikio pia kuuma na mara kadhaa alikuwa akisema alishindwa kupata usingizi kutokana na maumivu makali aliyokuwa akiyapata.
Chid ambaye msimu uliopita alicheza Coastal Union amesema, kuvunjika taya ndio jeraha baya alilowahi kupata kwenye maisha yake ya soka hadi sasa na kamwe hatoweza kusahau kabisa.
shaffihdauda.co.tz inaungana na familia ya Chidiebere, Stand United FC pamoja na wadau wote wa soka kumtakia kila la heri Chidiebere apone na arejee tena uwanjani.