Na Privaldinho Abiud
Tarehe 4 /12/ 2011 Raisi wa Brazil Dilma Rouseff alitangaza kuwa Brazil imepoteza mtu wa muhimu sana. Mji wa Belerm kule Para ulijawa na majonzi makubwa kutokana na taarifa ile ya Mh. Rouseff. Brazil ilimpoteza Socrates mchezaji nguli kabisa wa taifa hilo. Katika mji mdogo wa Igarapé-Açu, mzee Raimundo (baba yake Socrates) alikuwa maarufu sana, kutokana na cheo chake cha ukusanyaji wa mapato.
Mtoto wa kwanza wa Raimundo (Socrates) alikuwa ni mchezaji maarufu na wa kukumbukwa katika taifa lake. Socrates alisoma shule ya gharama kabisa kule Ribeirão Preto, Colégio Marista kutokana na kipato kikubwa cha baba yake.
Baada ya kushindwa Urais wafuasi wa George Weah waliingia mtaani kupinga matokeo. Baadhi ya viongozi wakubwa wa Afrika walimsifu George weah kwa kutuliza ghasia kwa kuwahimiza wafuasi wake wayakubali matokeo yale. George Weah alikuwa moja ya watu waliokuwa wakipinga vikali vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya taifa lile.
Socrates aliipinga Serikali ya kijeshi ya wakati ule iliyokandamiza sana soka katika taifa la Brazil. Socrates alihimiza wenzake kuvaa jezi zenye maneno ya Demokrasia. Alianzisha kikundi cha kisiasa kuitaka serikali kuandaa uchaguzi mkuu huru na haki. Harakati zile zilizaa matunda. Upendo wa mashabiki wa soka ulibadilisha serikali onevu. Zaidi ya Watu milioni moja walikaa nyuma ya Socrates kwa juhudi zake.
Bila shaka wachezaji wamekuwa na faida kubwa nje na ndani ya soka, kisiasa. Soka limeleta mahasimu wa UKAWA na CCM na wanageuka kuwa kitu kimoja pale uwanja wa Taifa. Soka linawafanya waislam na wakristo kuonesha maana sahihi ya ya msemo, sisi sote ni wamoja.
Nikukumbushe kitu kilichotokea mwaka 1969 ambacho kuna baadhi ya vyombo vinatoa tarifa tofauti tofauti. Pele alikwenda Nigeria na klabu yake ya Santos kwenye mechi za kirafiki dhidi ya timu ya taifa hilo. Nigeria kwa wakati ule palitawaliwa na vita dhidi ya jamii ya Biafra. Taarifa zinasema ndani ya saa 48 Pele aliyokuwa Lagos taifa zima zililitulia na vita vilisimama.
Watu waliweka tofauti zao pembeni wakiamini soka ndicho kitu pekee kinachowaleta karibu. Kiongozi wa chama cha michezo cha Nigeria Bw. A.B Osula aliwalipa Santos zaidi Paund 11,000 ili tu mchezaji bora wa dunia atue katika ardhi iliyokuwa imetapakaa damu.
Wakati Pele anawaachia amani Nigeria, upande wa pili kule Liberia George Weah mwaka huu huyoo anaelekea zake ikulu licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa Bokai ambaye alikuwa makamu wa Raisi, pamoja na swahiba wa Charles Taylor bwana Prince Johnson. Huyu Prince Johnson alikuwa kamanda wa kikundi cha waasai wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe vilivyochukua uhai wa waliberia zaidi ya laki 2 unusu.
Ikumbukwe mwaka 2012 Geroge Weah alikubali wito wa kuwa balozi wa Amani kumwakilisha aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi wa 2005 mkubwa Rais Sirleaf. Licha ya kulalamika kuibiwa kura lakini Weah bado aliamini katika amani. Bila kusahau mwaka 1997 Weah alitumia pesa zake mwenyewe kiasi cha dola milion 2 katika kuwasaidia watoto walioathirika na vita na alikuwa balozi wa UNICEF katika kupinga utumiaji wa watoto kama wanajeshi.
Weah ni mfalme wa soka katika taifa lake na Afrika kwa ujumla. Ametumia upendo wake katika soka ili kudumisha amani katika nchi yake. Ameonesha soka ni zaidi ya kuvaa jezi. Anajenga njia sahihi kwa wazazi wetu wa kiafrika ambao wanaamini soka ni uhuni. Wanasoka wana hamasa kubwa kisiasa. Wanyama alipokuja Bongo hakuna aliyemuuliza yeye chama gani, wala dini gani.
Furaha yangu ni kumwona mchezaji pekee mwenye Ballon d’Or kutoka Afrika akiwa Rais. Hata Raisi wa kwanza wa Algeria bwana Ahmed Ben Bella alikuwa kiungo hatari wa Marseille miaka 1940 kabla ya kuwa Rais wa nchi hiyo.