Mbeya City ‘timu ya kizazi kipya’ ilipanda kucheza ligi kuu Tanzania bara msimu wa 2012/2013 chini ya kocha Juma Mwambusi.
Timu hiyo iliwashangaza watanzania baada ya kufanya vizuri msimu huo na kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya tatu juu ya Simba ambayo ilimaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo.
Huu ni msimu wa tano Mbeya City ipo kwenye ligi, lajini tayari imeshabadilisha makocha wanne hadi sasa katika misimu tofauti. Hivi karibuni imemtangaza kocha mpya baada ya kuvunja mkataba na Kinnah Phiri, City ni sehemu salama kwa makocha?
Juma Mwambusi (2011-October 2015)
Aliiongoza City kupanda kutoka chini kabisaakaipandisha ligi daraja la kwanza hadi ligi kuu Tanzania bara akiwa na vijana wengi wageni VPL lakini alifanikiwa kuleta ushindani wa kutosha.
Deus Kaseke, Peter Mwalyanzi, Hassani Mwasapili na wengine wakisaidiana na akina Paul Nonga na Mwigane Yeya waliweza kufanya kweli chini ya Mwambusi.
Mwishoni mwa 2015 Mwambusi aliachana na Mbeya City na kujiunga na mabingwa wa kihistoria wa Tanzania klabu ya Yanga na kufanya kazi akiwa msaidizi Hans van Pluijm na baadae George Lwandamina kisha kuondoka kabla ya kuanza kwa msimu huu (2017/2018.)
Meja mstaafu Abdul Mingange (December 2015-2016)
Kuna wakati alikuwa msaidizi wa Mwambusi pale Mbeya City, kuonfoka kwa Mwambusi kukampa nafasi ya kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho pendwa cha wakazi wa jiji la Mbeya wenyewe wanaliita ‘Green City’.
Mingange hakufanikiwa sana akiwa kocha mkuu, mambo yalianza kumwendea mrama kutokana na wachezaji wengi wa kutumaini kutimkia kwenye timu nyingine za ligi kuu. Mwalyanzi, Kaseke, ni baadhi ya walioondoka na kujiunga Simba na Yanga.
Kuna wakati mashabiki wa timu hiyo walipaza sauti kumpiga Mingange wakitaka awaachie timu yao. Uongozi wa Mbeya City uliamua kuacahana na Mingange na timu kukabidhiwa Kijuso ambaye alikuwa msaidizi wakati ikifanyika mipango ya kupata kocha mpya.
Kinnah Phiri (February 2016-September 2017)
February 8, 2016 viongozi wa klabu ya Mbeya City walimtambulisha Kinna Phiri kwa waandishi wa habari kwamba ndiye kocha wao mpya atakaeifundisha klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miatatu.
Tofauti na makubaliano ya mkataba, Phiri hayupo tena Mbeya City baada ya mkataba wake kuvunjwa.
Mbeya City chini ya Phiri haikufanya vyema sana, msimu uliopita ilikuwa miongoni mwa vilabu vilivyosubiri hadi mechi ya mwisho kujua hatma yao kwenye ligi.
Kabla ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba Phiri alilalamika kutolipwa kwa miezi mitatu mfululizo na kusema anaidai Mbeya City zaidi ya Tsh. milioni 40.
Nsanzurwimo Ramadhani (October 2017…..)
Nsanzurwimo Ramadhani tayari amejiunga na Mbeya City kwa mkataba wa msimu mmoja, yupo na timu Kanda ya Ziwa kesho Ijumaa atakiongoza kikosi chake katika mchezo wa VPL dhidi ya Mbao kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Nsanzurimo amewahi kufundishavilabu mbalimbali kwa nyakati tofauti katika nchini za Burundi, Rwanda, Botswana, Malawi, Uganda, na Afrika ya Kusini.