Na Thomas Ng’itu
Wakati wa dirisha kubwa la usajili lilipokuwa linaendelea mwezi uliopita, nilikuwa najiuliza kwa nini Yanga wang’ang’anie kuwa Gadiel Michael ni mchezaji wao, huku yeye mwenyewe akiikataa Azam ghafla na kutaka kuondoka, Azam nao wakisema kuwa bado ni mchezaji wao halali kutokana na kuwa na mkataba na timu hiyo.
Mchezaji huyu hivi sasa amegeuka kuwa lulu, kati ya mabeki wanaocheza nafasi za pembeni kutokana na aina ya uchezaji wake.
Amkimbia Kangwa Azam
Gadiel aliona tayari kuna ufinyu wa namba katika kikosi cha Azam kutokana na kuwa na Mzimbabwe Bruce Kangwa hivyo ilipokuja ofa ya Yanga aliona bora aondoke.
Azam ilikubali kumuachia kwa kuweka dau dogo ambalo Yanga walitoa kama fidia na mchezaji huyo akajiunga na klabu hiyo ya Jangwani.
Kama bado angekuwa yupo mikononi mwa kocha wa Azam Cioba, inawezekana leo asingekuwa huyu tunayemuona, itakuwa aliona mbali zaidi na ndio maana akataka kuondoka, kikubwa ni kumuomba Mungu afanikiwe zaidi.
Ampora namba Mwinyi Haji
Ufalme wa Oscar Joshua ulichukuliwa na Mwinyi Haji, ufalme wa Mwinyi Haji umechukuliwa na Gadiel Michael hilo halina ubishi.
Michael amekuwa mchezaji wa adhimu tayari katika kikosi hicho kutokana na umahiri wake wa kumudu kuicheza namba hiyo.
Haji ana kazi kubwa ya kumshawishi Lwandamina ampe nafasi la sivyo yatamkuta kama yaliyomkuta Joshua kipindi yeye anacheza.
Lesotho yampa namba Stars
Mechi ya Stars dhidi ya Lesotho ndiyo ilikuwa mechi iliyofanya beki huyu apate namba ya kudumu Stars.
Alionyesha kiwango cha juu katika kukaba na kupeleka mashambulizi huku kikiwa ndio kitu sahihi katika mpira wa sasa (Modern football).
Mayanga ameonyesha kumuamini kijana huyu kutoka na kumpa nafasi kila anapomuita, Michael naye hajawahi kumuangusha.
Aina ya uchezaji wake
Amezidi kukomaa kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, amekuwa ni mchezaji mbishi dhidi ya washambuliaji pindi wanapokuja kushambulia lango lao.
Anapambana sana katika kuzuia mashambulizi lakini pia ni mchezaji ambaye anaweza kupeleka mashambulizi kwa spidi na kupiga krosi ambazo zinaweza kuzaa mabao.
Pia ana uwezo mkubwa wa kupiga faulo hasa za pembeni, hii ni kutokana na jinsi ambavyo anaweza kupiga krosi, hivyo faulo za pembeni anazitumia kama krosi zake.
Anasubiri tuzo ya chipukizi
Kwa umri alionao hivi sasa na kiwango ambacho anakionyesha, dhahiri kwamba anajipa wakati mwepesi katika kuingia kwenye kugombea tuzo ya mchezaji bora Chipukizi.
Kupata kwake namba katika kikosi cha Yanga na Stars, hii ni chachu kubwa kwani hata kwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ baada ya kufanya vizuri akiwa na Simba pamoja na Stars alijikuta akipata tuzo hiyo.
Nini afanye
Gadiel anatakiwa asilewe sifa kwani bado mapema mno kwake yeye kuona kama amemaliza kucheza soka, anatakiwa aangalie mbele zaidi.
Atengeneze muda mzuri wa kufanya mazoezi na kupumzika, kwani hiyo ndiyo itakuwa nguvu yake lakini pia awe na nidhamu ya kazi yake pamoja na watu ambao wanamzunguka.