Na Baraka Mbolembole
MOHAMED Mkopi alifungiwa kucheza soka kwa muda wa mwaka mmoja kutokana na kosa la kujisajili Mbeya City FC wakati angali bado na mkataba wa mwaka mmoja zaidi na klabu ya Tanzania Prisons.
Kutokana na adhabu hiyo iliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), kiungo huyo mshambulizi alishindwa kucheza msimu uliopita, ikiwa msimu mmoja baada ya kufanya vizuri yeye binafsi huku pia akiiisaidia Prisons kumaliza katika nafasi ya nne msimu wa 2015/16.
Wakati, Mkopi akitenda kosa hilo na kupewa adhabu, City wao hawakuguswa na lolote japokuwa mikataba ya wachezaji wote ipo katika TMS. Hadi kufikia hatua ya kuzungumza na mchezaji aliye katika mkataba wa zaidi ya miezi sita pasipo kuishirikisha klabu yake, ni dhahiri hilo ni kosa kubwa, na klabu husika inapaswa kupewa adhabu.
TFF izifungie kusajili klabu zinazowasaini wachezaji wenye mikataba na timu nyingine
Lakini jambo la ajabu ni pale TFF inapochukua hatua kwa wachezaji pekee na kuviacha vilabu ambavyo huenda kuwarubuni wachezaji hao. Katika nchi zilizoendelea katika mtazamo wa soka la kulipwa, City ingekuwa imepewa adhabu kwa kosa la kumsaini mchezaji aliye katika mkataba na klabu nyingine pasipo kuishirikisha klabu yake. Hii haipaswi kutazama mazungumzo na makubaliano ya Mkopi na City kwa sababu wote walitenda kosa.
Kwa nini TFF hushindwa kuzipa adhabu klabu zinazowasaini wachezaji wenye mikataba na klabu nyingine? Ni ushabiki kupitiliza labda walionao watendaji wa juu wa soka la Tanzania kwa baadhi ya timu wanazozishabikia. Kama sivyo inakuwaje sajili za Mbaraka Yusuph kutoka Kagera Sugar kwenda Azam FC, Aishi Manula kutoka Azam FC kwenda Simba SC zilikamilika licha ya makosa yaliyofanywa na ‘klabu nunuzi.’
Mchezaji anaweza kusaini makubaliano ya awali na klabu nyingine ikiwa mkataba wake utakuwa chini ya miezi sita. Kusaini mkataba rasmi ni kosa na inapotokea kosa hilo adhabu zinapaswa kuwahusu ‘wafanya makosa wote’ kwa kuwa mikataba ya wachezaji iko wazi katika TMS. Klabu haipaswi kuingia mkataba na mchezaji aliye katika mkataba na klabu nyingine hata kama mkataba huo umesalia masaa kadhaa kabla ya kumalizika kwake, vinginevyo ni biashara.
Inashangaza sana kuona TFF ikiadhibu wachezaji pekee
Pius Buswita na kuicha klabu ya Simba bila kuipa adhabu yoyote. Ukifuatilia wasemavyo viungozi wa Mbao FC, Buswita mwenyewe, meneja wake, na uongozi wa Yanga SC utagundua Simba inapaswa kupewa adhabu sambamba na mchezaji mwenyewe kama kweli mchezaji huyo aliyeng’aa akiwa na Mbao FC msimu uliopita alisaini mikataba na klabu mbili za Simba na Yanga.
Watu wa Mbao wanasema wanachofahamu wao ni kwamba, Yanga iliwafuata na kuulizia kuhusu upatikanaji wa Buswita. Wakaambiwa mchezaji huyo bado ana mkataba na Mbao. Biashara ikafanyika baina ya pande mbili Mbao FC na Yanga, huku meneja wa mchezaji na Buswita akiwepo.
Hii ilikuwa biashara salama na ya kuigwa katika nchi ambayo inapambana kuelekea katika soka la kulipwa. Yanga walimsajili kihalali mchezaji huyu baada ya biashara na klabu iliyokuwa ikimmiliki. Wakati unamaliza biashara nzuri na ya haki, unategemea kuona majibu ya mchezaji husika ndani ya uwanja, ila ghafla unaambiwa mchezaji huyo amesaini timu nyingine.
Simba imemnunua wapi Buswita?
Bila shaka watajibu Mbao FC kwa sababu ni timu aliyokuwa akichezea Buswita msimu uliopita. Ukiwauliza mkataba wao wamesaini na nani, watajibu na Buswita. Pia ni jibu zuri. Nikiwauliza swali la tatu,je walimsaini mchezaji huru au aliye katika mkataba na Mbao FC wataanza kubabaika na mwishowe watajibu, ‘mchezaji alituambia amemaliza mkataba’
Je, hivi ndivyo inavyopaswa kuwa? Siwalaumu viongozi wa sasa klabuni hapo kuhusu uhamisho wa Buswita kwa sababu wao walikuta tayari mambo yameshafanyika na wale wajuzi wanaokaimu nafasi zao hivi sasa. Lakini naamini klabu hiyo inapaswa kupewa adhabu sambamba na Buswita kutokana na kosa la kumsaini mchezaji aliye katika mkataba na klabu nyingine.
Nani asiye na tamaa ya pesa?
Ni wachache sana wenye ujasiri wa kuikataa pesa usiyowahi kuishika hasa pale inapokujia ghafla kutokana na kipaji chako, kazi yako. Leo hii Buswita anaweza kuonekana mtu mwenye tamaa ya pesa kiasi cha kuwahadaa Simba na kufanya udanganyifu katika mkataba wake na Mbao FC, lakini isisahauliwe kuwa Simba ilikwenda kumuhadaa na kumsainisha mchezaji huyo angali katika mkataba na Mbao FC.
Kama walisaini makubaliano ya awali tu iweje mchezaji afungiwe wakati hili linaweza kuwa sawa na kesi ya madai tu. Simba itadai ilichompa mchezaji na mchezaji atalipa lakini kama walimsainisha kabisa mchezaji hapo ndipo ambapo nataka kuona TFF ikichukua hatua pia kwa Simba kwa maana walimsaini mchezaji aliyekuwa katika mkataba na timu nyingine.