Quantcast
Channel: Makala – ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

Ngumu Kumeza ya September 1, 2017 imegusa wapi? Kama ilikupita isome hapa…

$
0
0

Unaweza kuwaita makaidi, jeuri na mengineyo lakini  hawajawahi kusajili mara mbili, hapo nawazungumzia Haruna Moshi ‘Boban’ na Athumani Idd ‘Chuji’ pamoja na utukutu wao walibaki kwenye kuheshimu saini zao pamoja na kuheshimu alama zao za vidole.

Inasikitisha kuona kijana anawaza kama mzee, inapunguza hata ari ya kutupa shuka ukiona dunia inaenda kasi kulia wengine wanarudi kusho na inakatisha tama kusikia wakala anaomba busara wakati yeye ni mmoja ya watu haribifu waliosaidia kupotosha ukweli kwenye mpira.

Sauti inayotoka kwenye radio inasema, ‘mchezaji alipitiwa na shetani tumsamehe’ maana shetani ana nguvu ya kumshurutisha kiti. Nauliza tu mtabora umeshawahi kuwa mganga wa dawa za kienyeji? Elimu ni muhimu sana, kutojitambua ni mzigo haina tofauti na kuwa na koti kubwa kama mende lakini bado makazi yako uyafanye ya msalani.

Muwamba ngoma anavutia kwake na ndio hapo Mkwasa anajigeuza muwamba ngoma na kuanza kuvutia kwake kuwa wao wamemsajili Buswita wakati Simba wamemsajili Buswata. Ukifikiria kwa ukubwa unagundua kuwa ile ni michezo michafu ya wachezaji wasiojitambua. Ndio utakuta wanabadili herufi kadhaa kujitofautisha na saini ya upande mwingine.

Haya yanatokea huku kwetu kwenye giza na shirikisho linayabariki kwa kuyaundia kamati za kusikiliza hoja za kijinga na upuuzi. Tunaambiwa muda ni fedha sasa hivi kamati kweli isikilize hoja dhaifu kama hii ‘mama alitishiwa ndio maana nikasaini’ je mlifungua jalada kituo cha polisi Butimba kama sio Kirumba? Lazima atajing’ata hapo.

Wengine wanatokea kutetea kupitia hoja ‘mbona majina yapo tofauti’, wengine wanakuja na hoja isiyo na afya ‘mbona hakuwekewa pingamizi’. Ulaya huko dirisha limefungwa hatusikii mvutano wowote kuhusu usajili kwa vile wameweka mambo yao bayana na sheria zinafuatwa. Unakumbuka usajili wa De Gea kwenda Madrid ulivyo kwama dakika za mwisho kwenye mabadilishano ya nyaraka? Ingekuwa huku Bongo, watu wangeomba busara itumike siku ziongezwe.

Unakumbuka usajili wa Fabio Contrao ulivyoshindikana kwenda Manchester United? Ingekuwa huku kwetu muda wa usajili tungeongeza na vikao vya kamati za kahawa vingepewa muda wa kupitia hizo pingamizi. Huo muda wa hizo kamati kukaa kupitia majina ni ishara ya kuwatengenezea watu namna ya kufika maliwatoni, hakuna lingine mbona nchi nyingine mpira unachezeka bila kelele wala hayo mapingamizi?

Mikataba ikisainiwa na vilabu kivuli kinapelekwa TFF, sasa kuna haja gani vivuli vya kandarasi zinazoonesha muda uliosajiliwa na mpaka utakapoisha mpewe na bado mshindwe kuamua kesi zisizo na kichwa wala miguu. Kuna watu wanaomba busara itumike mimi nawaambia endeleeni kutumia busara hata kuamua vitu vya kipuuzi, ni matumizi mabaya ya busara hali hiyo ndio imetufikisha kisiwa hiki  ambacho Rais wa awamu ya pili alikiita ‘kichwa cha mwendawazimu’.

Amlima aliwahi kusaini vilabu vitatu kisha akatoweka alijua alichofanya na alisubiri mpaka adhabu yake ilipomalizika ndipo akaruhusiwa kucheza tena. Alichofanya Buswita sio jambo jipya ni vitu vya kale na inatosha kusema yeye na meneja wake hawajapevuka kimaamuzi.

Dua zetu kwa Mungu zisilenge sana kuomba atuwezeshe kwenye rizki tuombe pia atujalie kufanya maamuzi ya busara, mwanzoni mwa mwezi wa sita Buswita alitumiwa tiketi ya ndege kutoka Mwanza kuja Dar na kupokelekewa na viongozi wa Simba na baada ya hapo walikaa na kumaliza suala zima la usajili.

Majuma machache baadae mmoja wa wadau wa Yanga alikwenda Mwanza na kuongea na Buswita pamoja na Salmin Hozza ambaye pia usajili wake ungekuwa na utata endapo Azam na Yanga wasingekaa chini kwenye usajili wa Gadiel Michael. Huenda mwanaharamu asingepita na Hozza pia angeenda na maji.

Kwa mujibu wa Mkwasa Salmin Hozza nae sijui alikutwa wapi mpaka shetani akampitia na kusaini Azam na Yanga kabla ya Yanga ‘kuufyata’ kwa Azam na kuuchana mkataba wa Hozza, vinginevyo tungeshuhudia mengi.

Ngosha ananiambia usiache mbachao kwa msala upitao, ujue Buswita aliponzwa na milioni 20 za Yanga dhiai ya milioni 10 alizochukua Simba ndio maana haya yanatokea, kwa hiyo mwache ale matunda ya upumbavu wake. Mchuma janga hulia na wa kwao, wengine jifunzeni kupitia huyu maana huu ndio mfano halisi na rahisi wa mwenye kiranga haliliwi hata akifa hawekewi matanga.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>