Na Baraka Mbolembole
UIMARA wa Yanga SC katikati ya uwanja , nidhamu ya hali ya juu kutoka kwa wachezaji, na uwezo wa kukaba, kuipeleka timu mbele, na uamuzi wa haraka wa kiungo, Mcongoman, Papy Tshishimbi ulichangia kwa kiasi kikubwa ‘yale matarajio’ makubwa ya Simba SC kuishinda Yanga ndani ya dakika 90’ yakiyeyeyuka, na sasa kinachozungumzwa ni uwezo wa chini kiufungaji wa kikosi cha Mcameroon, Joseph Omog.
Kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya mahasimu wa soka nchini Yanga na Simba siku ya Jumatano hii, ni wazi katika makaratasi Simba ilikuwa na kikosi ‘kabambe’ kuliko na hali hiyo ilipelekea baadhi ya wana Yanga kuamini timu yao ilikuwa ikienda kupoteza na pengine kuambulia kipigo cha aibu kutoka kwa ‘watani wao jadi.’
Licha ya kushindwa kupata ushindi katika mchezo wa nne mfululizo katika ‘Dar es Salaam-Pacha’ Yanga wanaweza kuendelea kujivunia kikosi chao kuelekea msimu mpya wa ligi kuu Tanzania Bara. Kocha wa timu hiyo, George Lwandamina anaweza kufanikiwa zaidi katika timu hiyo kama ataweza kutengeneza timu imara.
Inawezekana Lwandamina alikuwa akibebwa na wachezaji bora katika klabu yake ya zamani Zesco United ya Zambia. Ndiyo timu yake ya sasa haiwezi kutengeneza nafasi nyingi za kupata magoli. Timu yake ilionekana kutoka vizuri nyuma ikiwa na mpira, lakini walishindwa kutengeneza nafasi na kupiga pasi nzuri za mwisho ili kupata magoli.
Katika mchezo wa jana sijaona kipya kutoka kwa kocha huyo lakini uwezo wa wachezaji wake wapya, golikipa Mcameroon, Youthe Rostand, mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael, viungo wa kati, Mcongoman, Tshishimbi, Rafael Daud na mshambulizi Ibrahim Ajib ambao wote walianza katika mchezo huo wanaweza kumuongezea mbinu.
Lwandamina ni mzuri katika mbinu za kuzuia, lakini anaweza kuwatumia Tshishimbi na Mzimbabwe, Thaban Kamusoko kutengeneza kiungo ambacho kitahusika pia katika kutengeneza magoli kwa safu yao ya mashambulizi.
Uwezo wa kuziba nafasi na kukaba, kupiga pasi na kubaki katikati ya uwanja ulioneshwa na Tshishimbi katika mchezo dhidi ya Simba ulimpatia uhuru wa kusogeza timu mbele Kamusoko. Namna wawili hao (Kamusoko na Tshishimbi) walivyoweza kuwazima viungo watano wa Simba ni ishara kwamba muhimili wa kikosi cha Lwandamina utakuwa wao. Na lazima awatumie vizuri, yupi ashambulie na yupi acheze kwa kuzuia na kushambulia kwa kustukiza.
Inawezekana safu ya washambuliaji Ibrahim Ajib na Mzimbabwe, Donald Ngoma haikutengeneza nafasi ili lilitokana na kwamba washambuliaji hao wawili wote wanapendelea kucheza kwa kuhamahama, na hii ni changamoto kwa Lwandamina kama atashindwa kumtumia Mrundi, Amis Tambwe kama mshambulizi wa kati.
Mchezo wa Ngao ya Jamii umewaondoa hofu mashabiki wa Yanga ambao walikuwa na wasiwasi hasa baada ya timu hiyo kuwapoteza wachezaji kadhaa muhimu katika kikosi ambacho kiliwapa taji la tatu mfululizo msimu uliopita.
Tshishimbi ameonesha anaweza kuzibavizuri nafasi iliyoachwa na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, huku Vicent Andrew akionesha dalili nzuri za kuchukua nafasi iliyoachwa na Mtogo, Vicent Bossou kama wakongwe, Kelvin na nahodha Nadir Haroub watashindwa kugangamara.
Lwandamina tayari ameanza kufanikiwa kwa kuifanya Yanga icheze kama timu, lakini hilo halipasi kupunguza ufanisi wa timu katika ufungaji na anachopaswa kufanya sasa ni kutengeza pacha zinazoweza kucheza pamoja katika safu yake ya washambuliaji sita.
Lwandamina anapaswa kuwajenga nyota wake hawa na kupata pacha nzuri katika ufungaji, Tambwe, Mzambia, Obrey Chirwa, Matheo Anthony ambao hawakutumika katika mchezo wa jana na Ngoma, Ajib na Emmanuel Martin ambao walianza katika kikosi cha kwanza vs Simba.
Utulivu, ukomavu, na utatari wa wachezaji wa Yanga waliouonesha vs Simba inatoa ishara njema kwa timu hiyo kuwa inaweza kushinda ubingwa wa nne mfululizo msimu huu.
Nimemuona Gadiel akiongeza nguvu ya kuzuia na kushambulia katika beki tatu, Daud anahitaji kujiamini tu, Ajib anapaswa kujenga utulivu, lakini sina cha kusema zaidi kwa sasa kuhusu Tshishimbi ila nimemuona ‘mtu mpya’ anayeweza kuipeleka mbele zaidi Yanga SC.