Quantcast
Channel: Makala – ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

Kisima Cha Barcelona na Miguu Ya Neymar Ndani Yake.

$
0
0

Ndani ya ubongo wa kocha wa timu ya Taifa ya Brazil, Tite anaamini kuwa hakuna mchezaji aliyekuwa kwenye kiwango bora zaidi ya Neymar kwa sasa. Kwake miguu ya mchezaji huyu ndiyo yenyewe thamani kubwa kwa sasa na ambayo inafanya vitu ambavyo wengi wanaweza kuita ni bidhaa zisizopatikana sokoni yaani adimu.

Ni Neymar huyu ambaye wakati Messi ameamua kuchukua likizo yake ndani ya uwanja dhidi ya Paris St Germain aliamua kubeba msalaba wa moto na kuivusha Barcelona kwenda ng’ambo inayofuata. Kiwango alichokihamishia timu ya Taifa mpaka wanakuwa timu ya kwanza ya Taifa kufuzu kwenda kombe la dunia kule Urusi.

Inawezekana asionekane kwa kiasi kikubwa kwenye orodha ya juu ya wafungaji kwenye ligi kuu ya nchini Hispania, La Liga msimu huu, lakini pia unaweza kumtaja kama mchezaji muhimu zaidi wa klabu ya Barcelona kwa sasa na usipingwe.

Huyu ndiye haswaa aliyeshikilia funguo za Barcelona kama tu watataka kufungua mlango wa paradiso na huyu ndiye maji sahihi kwenye udongo wenye rutuba pale Camp Nou. Haipingiki kuwa hakuna binadamu mwenye kofia kichwani kwake ndani ya Barcelona zaidi ya Lionel Messi, huyu ndiye Daudi wao yaani mfalme wa wafalme wengi wanaopatikana hapo ndani.

Upofu pekee ndio unaoweza kumfanya mtu asitizame miguu ya Neymar ndani ya uwanja kwa sasa. Pamoja na Messi na Suarez kuwa na wastani mzuri wa mabao, bado Neymar ndiye anayeamua sumu yao hawa wawili isambae kiasi gani kwenye mwili wa adui. Neymar ndiye anayeamua kasi ya timu na namna ipi timu inaondoka kuelekea mbele.

Bahati mbaya ni kuwa usajili wa Barcelona uliopita ambao ulishuhudia Andre Gomez ambaye alitegemewa kuja kupunguza mzigo wa Iniesta, Pablo Alcacer ambaye angeweza kushusha pumzi za Messi na Suarez na pia Denis Suarez ambaye alikuwa mtoto anayetegemewa kukua haraka wote hawajaweza kufikia matarajio na maswali yaliyokuwa kwenye karatasi zao yalikuwa mtihani mgumu usiojibika kirahisi kwao.

Usingizi aliolala pono siku zote hutakiwa kuwa manufaa kwa mvuvi kwa sababu hatumii nguvu nyingi, lakini kwa Barcelona kwa siku za karibuni imekuwa tofauti. Walikuwa Simba waenda pole lakini nyama aliyoamua kuiacha Real Madrid wala hawajataka kusumbuka kuitafuna, na ndio kwanza Malaga walionekana klabu kubwa isiyokabika.

Baada ya Real Madrid kupata sare dhidi ya waliozaliwa nao pamoja Atletico Madrid, ilikuwa ni kazi iliyozoeleka ambayo Barcelona walitegemewa kuifanya dhidi ya Malaga. Lakini maisha yakawa tofauti, na ugumu wake ukapelekea Neymar kupewa kadi nyekundu aliyostahiki.

Punda ukimtuma sana hulala akiishiwa nguvu, ndivyo unavyoweza kutafsiri maamuzi ya Neymar, katika hatua muhimu kama hiyo, ni wazi presha ilikuwa juu yake na akashindwa kumuda mchezo. Lakini mdomo huponza kichwa, kitendo cha kuonekana kumdhihaki mwamuzi maana yake kimemfanya afungiwe michezo 3, ikimaanisha atakosekana dhidi ya Real Madrid kwenye El Clasico, huku ikiwa na tafsiri pia kuwa, Barcelona watacheza mchezo huo na mguu mmoja.

Inawezekana kabisa hii ikawa chungu kwa klabu lakini shubiri kwa mashabiki, dozi yao haitofautiani sana. Kumkosa Neymar kwa kipindi hiki kwa Barcelona ni kuepuka kutumia mwiko katika kuivisha ugali, tena msukuma ndiye mpishi. Kuuivisha inaweza kuwa tatizo kiasi lakini kuupika nao ni uamuzi mgumu.

Kwa sasa inaonekana kuwa tatizo la kawaida, inaonekana kuwa jambo lisilokuwa kubwa lakini hii ni furaha ndani ya Real Madrid. Adui kapata njaa na vita yake inakuwa ngumu kiasi, hii inamaanisha kuwa Lionel Messi itabidi abebe mzigo kwa sababu huwezi kumtuma Suarez kufanya kazi ya Neymar.

Kasi ya Neymar, ubunifu na wingi wa mabeki anaoweza kuwavuta upande wake imekuwa silaha ambayo inamfanya asifunge kwa kiasi kikubwa lakini ndio inayomfanya kuwa mchezaji aliyepewa alama nyingi zaidi kwenye michezo mingi kwa sababu anafanya kazi kuwa rahisi kwa pacha wenzie waliosalia.

Hii ndio sababu pia katika michezo ambayo haonekani kucheza vyema basi na Barcelona wanapoteza ubora wao. Juventus walilijua hili na wakahakikisha hachezi, na Barcelona ikafa. Messi hawezi kuwa yule wa siku zote wa kuisukuma timu. Miguu ya Neymar inahitajika.

Umefika muda ambao watu inabidi washike tama, umefika muda amabo mashabiki wa Barcelona wanaweza kuanza kununua dawa za maumivu. Kama machozi yapo jirani basi unaweza kuwa muda sahihi wa kuyaachia yatiririke. Ondoa machungu yamalizike kwa sababu Neymar kachafua kisima na Barcelona inaweza kuwabidi kukata kiu kwa maji yasiyokuwa safi na salama. El Classico haiwezi kuwa nyepesi bila Neymar, amekuwa chumvi katika kila mboga iliyopikwa na Barcelona msimu huu.

 

 

 


Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>