Quantcast
Channel: Makala – ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

Jicho la 3: Jerry Murro aliipeleka ‘Yanga moja’ uwanjani, Manara anawagawa Simba kila mechi

$
0
0

Na Baraka Mbolembole

“Uwezo wa Kamusoko ni sawa na viungo watatu wa Simba…” ni kauli iliyoendana na ukweli, na mtamkaji (Jery Muro) alimaanisha kile alichokiona Februari 2016 wakati kiungo huyo raia wa Zimbabwe, Thabani Kamusoko alipowavuruga Simba SC na kuisaidia timu yake ya Yanga SC kushinda 2-0 dhidi ya mahasimu wao hao na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara msimu uliopita. Alikuwa sahihi asilimia 100.

“Baada ya Diamond na Ally Kiba, Ibrahim Ajib ndiye anayefuata kwa utoaji wa burudani nchini…,” ni maneno ya mkuu wa kitengo cha habari klabuni Simba, Haji Manara mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Tanzania Bara na Burundi siku ya Jumanne iliyopita. Alikuwa sahihi asilimia 0.

Kwanini nimenukuu kauli hizi? Kuzaliwa katika familia ya soka kuna faida na hasara zake. Na wakati mwingine mtu alinayetokea mahala kusiko na historia ya kimpira anaweza kukupatia faida kubwa zaidi kuliko yule anayetokea familia ya soka.

Kuanzia wakati wa Louis Sendeu na Baraka Kizuguto, Yanga imefanikiwa kupata watu sahihi katika kitengo cha habari, lakini misimu miwili ya Jery Muro kama Ofisa habari wa klabu hiyo, klabu imejengeka kama timu. Jery japokuwa alibezwa sana na kuambiwa hajui chochote kuhusu soka alitumia-taaluma yake, ushawishi wake na kipaji chake cha uzungumzaji kuifanya Yanga kuwa ‘timu moja.’

Wakati huu akiwa anatumikia adhabu ya kutojihusisha na soka kwa muda wa mwaka mmoja, naiona Yanga ikikosa huduma yake. Mwenyeji huyo wa Kilimanjaro aliwafanya wapenzi na hata wale wasio wafuatiliaji wa soka kutazama TV/kutegea sikio – radio zao na kumsikiliza kila anaposikika ama katika Tv wakati anapofanya mahojiano na wanahabarii. Hata wana-habari walipenda kufanya mahojiano na Jery
kutokana na kutoa maneno yaliyoleta ‘mshawashwa’ kwa mashabiki wa soka.

Alipokuwa akizungumza kuhusu kikosi cha timu yake, Jerry alizungumza kishabiki sana, lakini maneno yake mengi yalijaa hamasa-akiwahamasisha mashabiki, wanachama, wachezaji, benchi la ufundi na uongozi. Alirusha ‘madongo’ mazito kwa wapinzani wao na bila kujali Yanga ilikuwa ikiienda kucheza na timu gani yeye alipendelea kuzungumzia ‘uelekeo’ wa mchezo husika.

Hakuacha ‘kuikejeli’ Simba, ila alifanya dhihaka kwa mahasimu wao hao baada ya kuchunguza madhaifu yao. Aliwakejeli kwa kushindwa ‘kupanda ndege’ kwa misimu minne mfululizo-akimaanisha kushindwa kuiwakilisha Tanzania katika michuano yoyote ya Caf baada ya kushindwa kufanikiwa katika michuano ya ndani.

Wakati aliposimama katika taaluma yake,Jerry alikuwa ‘mtu smart sana’ na alizungumza kiuweledi-mfano wakati ule ilipotangazwa kufukuzwa kwa kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ksha kurudishwa kwake Jerry alisimama kama mkuu wa kitengo cha kuwajuza habari wana-Yanga na jamii kwa ujumla kuhusu kila kilichokuwa kikifanywa na uongozi.

Aliikingia Yanga kifua tena kwa hoja zenye mashiko kila TFF ilipoijia juu klabu hiyo. Muro alifungiwa mwaka mmoja na TFF kwa sababu tu alitetea kitendo cha klabu yake kuingiza watazamaji 40,000 bila malipo katika pambano la Confederation Cup June, 2016 kati ya Yanga v TP Mazembe.

Kwanini Jerry ni pengo kwa Yanga hivi sasa? Ni pengo kwa maana Yanga inakwenda kucheza michezo yake hivi sasa huku shabiki, mwanachama, mchezaji, kocha na kiongozi akiwa na mtazamo wake kuhusu uwezo wa timu yao.

Nakumbuka mara baada ya Yanga kuchapwa na Coastal 2-0, kisha kulazimisha sare ‘tata’ dakika za mwisho vs Tanzania Prisons, na hata pale walipokuwa nyuma kwa alama zaidi ya 7 dhidi ya Simba msimu uliopita lakini bado Yanga hawakupoteza umoja, hamasa, matumaini na uaminifu kwa kikosi chao kutokana na maneno ya kutia moyo kikosi chao.

Wakati wa usemaji wa Murro klabuni Yanga kuanzia mashabiki, wanachama, wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wote walikuwa wakienda kuitazama timu yao wakiwa katika lugha moja “tutashinda.” Na mara nyingi walifanikiwa, na walikuwa wamoja na tumaini moja kutokana na hamasa ambazo zililetwa na Muro.

HAJI MANARA

Historia ya soka la Tanzania inamtaja Sunday Manara kama mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza soka barani Ulaya, kwa wale waliopata kumuona Sunday akicheza wanamtaja kama mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania na alipewa jina la ‘Computer’ hata kabla hazijaanza kuingia nchini-sijui kwa maana nimasimulizi tuliyoyakuta.

Sunday ndiye baba mzazi wa Haji Manara ambaye sasa ni msemaji wa klabu ya Simba tangu Julai 2014. Haji alichukua nafasi ya Asha Muhaji ambaye alikaimu kwa muda nafasi iliyokuwa imeachwa na Ezekiel Kamwaga. Cliford Ndimbo ndiye msemaji wa kwanza wa klabu hiyo na hadi sasa Haji ni mtu wa nne kushika wadhifa huo.

Tofauti na Ndimbo, Kamwaga, Asha Muhaji, huyu Manara  ni mtu anayetoka familia ya mpira zaidi na iliyopata mafanikio makubwa, nasikia naye alipata kucheza soka katika wakati wake. Lakini mbona sioni mchango wake kwa klabu tofauti na ule wa Muro, Ndimbo, Kamwaga, Asha ambao hawajatoka katika ‘familia staa za soka?’

Niwe mkweli, sijawahi kushabikia maneno yake ya nje ya uwanja, hamasa zake na uwezo wa kuiunganisha Simba kuwa timu moja-kwa maana kuanzia kwa mashabiki, wanachama, wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wote wanakuwa katika ‘mwelekeo mmoja.’

Nadhani hata baadhi ya wakereketwa wa klabu ya Simba HAWAPENDEZWI NA UTENDAJI KAZI WA Manara kwa maana ya kutoa taarifa zenye mwelekeo sahihi wa mchezo unaohusu timu yao. Manara amekuwa maarufu kwa kutengeneza picha za watu na kuwafananisha na baadhi ya wachezaji wa Yanga kuliko kufuatilia mapungufu yaliyopo katika timu nyingine.

Huwezi kuwa na ‘cha-kuwabeza’ Yanga hivi sasa kwa maana wapo katika mwelekeo sahihi kwa msimu wa nne sasa. Kuisema vibaya ni sawa na ‘mtu avuae nguo na kushindwa kuchutuma kwa maana atajitukanisha mwenyewe kwa kwenda uchimbele za watu.’

Yanga wapo katika wakati mgumu hivi sasa kutokana na kumkosa Muro, timu kuandamwa na majeruhi, huku hamasa na viwango vya baadhi ya wachezaji wao vikiwa vimeshuka. Lakini kama timu iliyokuwa kwenye ubora inajitahidi kupambana kumaliza ligi  katika mwelekeo  mwingine lakini kwa nia ileile ya kushinda ubingwa wa watatu mfululizo.

Huu ulikuwa wakati sahihi wa Manara kujaribu kuwashawishi wana-Simba na kuwahamasisha katika ukweli ili wawe na tumaini moja. Kuwashutumu hovyo waamuzi, kuzungumza maneno yasiyo na ‘kichwa/miguu wala mwelekeo wa mechi’ ni baadhi ya mambo ambayo yanashindwa kutengeneza umoja wa klabu na Manara hawezi kukwepa kuwa kinara wa hili.

‘Kuiga si ujinga’ hasa pale unapoiga kizuri kinachoweza kukujenga, Haji amuige Muro ambaye aliwapa jeuri wana-Yanga na Yanga ilimpa jeuri kutokana na meneno ya hamasa yaliyokuwa yakisambnazwa na Muro.

Simba bado wana safari ndefu kufikia kushinda ubingwa wa kwanza wa VPL tangu msimu wa 2011/12 na kwa kuwa haina mwendelezo mzuri katika kupata ushindi hasa michezo ya mwisho wa msimu, Haji anapaswa kuhamasisha timu yake na si kutoa kejeli ambazo haziendani na Yanga licha ya kwamba ni ‘Watani.’

Muro aliipigania Yanga ili mechi zake zisogezwe mbele na TFF kutokana na ratiba ya Caf, licha ya kubezwa kuwa si mtu wa mpira lakini mawazo yake yaliendana na hali halisi. Manara yeye amekuwa akiishinikiza TTF kusimamisha mechi zao wakati timu inashinda mfululizo kwa sababu tu walingane michezo na Yanga na Azam FC.

Kwa mtu wa mpira hii ni aibu kwa maana anaonekana hajui kuwa timu inaposhinda mfululizo hujiamini zaidi na wapinzani wao kujenga hofu. Manara amekuwa mstari wa mbele kushinikiza TFF ipange waamuzi sahihi katika mechi zao kama vile timu nyingine zina waamuzi wao!

Manara ni tatizo Simba na Jerry ni pengo kubwa katika klabu ya Yanga japokuwa wanajitahidi kuliziba. Jerry Muro aliipeleka ‘Yangamoja’ uwanjani, Manara anawagawa Simba kila mechi kwa kuwaaminisha mambo yasiyokuwepo, yasiyotarajiwa na yasiyo na mwelekeo wa mechi husika. Kuna wakati anapaswa kuzungumza kiuweledi.

Jerry aliwafanya Yanga kuwa wamoja lakini ukichunguza kauli za Manara, mfano Januari mwaka huu aliposema Emmanuel Okwi atacheza vs Yanga Februari 25 ni kielelezo tosha kuwa licha ya kutoka familia ya soka, Haji si mtu mwenye uwezo wa kuutazama mpira na kung’amua mapungufu ya timu yake na wapinzani. Amuige Jerry Murro.

Jery aliwaaminisha Yanga na mchezaji husika kuwa ‘Kamusoko mmoja ni sawa na viungo watatu wa Simba kiuwezo’ lakini Haji anawaaminisha Simba kuwa Ajib ndiye mburudishaji bora zaidi nchini baada ya wanamuziki Diamod Platnum na Ally Kiba!!!


Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>