Na Abdul Mkeyenge
MOJA ya nukuu ninazozipenda ni ile inayosema ukimuelewa Mwanamke umeielewa dunia. Hii ni nukuu inayopendwa kutumiwa na rafiki yangu Ally Kamwe katika maandiko yake matakatifu. Dunia ya leo sio ya kumuelewa kila mmoja. Ukiuelewa ubavu wako basi umeielewa dunia.
Mijadala ya Mrisho Ngasa kurejea nyumbani na kuamua kuachana na Fanja ya Oman imekuwa mingi kwenye mitandao ya kijamii kuliko mijadala ya kujiuliza hali ngumu ya maisha tuliyokuwa nayo. Kila mmoja ana mtazamo wake na urejeo wa Ngasa. Hakuna anayewazia ugumu wa maisha yaliyofanya biashara ya pochi kwa Machinga kuwa ngumu mtaani. Leo hii unanuna pochi ili uweke nini?
Katika ugumu huu wa maisha tulionao Watanzania tumejisahaulisha kwa muda na tumemgeukia Ngasa kujiuliza maswali mengi ambayo majibu ya maswali yetu anayo Ngasa mwenyewe. Kama ana majibu sahihi ya kutupa juu ya maswali yetu, sisi kina nani mpaka tuanze kubishana nae na kumnyooshea vidole kila anapokatisha mtaa mmoja kwenda mwingine?
Ngasa anafanya kitu anachojua faida na hasara zake. Haya maamuzi yake ya kusaini ndani ya timu na kucheza mechi mbili kisha kuvunja mkataba hafanyi kwa makusudi au bahati mbaya. Anajua anachofanya. Passport ‘Hati yake ya kusafiria’ inaonesha amezaliwa mwaka 1989 kwa maana ana miaka 27. Mtu mwenye miaka 27 bado wa kumshangaa kwenye maamuzi anayoyasimamia? Tumuache afanye anachokiona sahihi. Si lazima wote tumuelewe. Kujielewa mwenyewe inatosha.
Mpaka mwaka 2016 ukibakiza siku 16 uweze kumalizika na kuingia 2017, fahamu Ngasa amecheza timu tatu tofauti. Amecheza Free State, Fanja na sasa yuko Mbeya City. Unadhani Ngasa hajui hiki anachokifanya mpaka kila mmoja kuinua mdomo juu na kuropoka anachojisikia? Anajua sana, sisi wengine tusimame nyuma yake na kuiheshimu akili yake inayoamua. Kama tunaweza kuiheshimu miguu yake ya dhahabu anapokuwa ndani ya dimba inakuwaje tunaibeza akili yake nje ta dimba?
Ngasa akiwa uwanjani anakuwa na akili za ‘Ki-messi-messi’. Lakini nani anayejua kama yeye ni mtu mahiri wa kujisimamia masuala yake ya nje ya uwanja kwa maana kuvunja na kusaini mikataba minono? Kuwa mchezaji mahiri na kuwa mtu mahiri unayeweza kujisimamia katika masuala ya mikataba ni kazi mbili tofauti. Lakini anachonifurahisha Ngasa ni kuzifanya kazi zote hizi bila shida na yake yakimuendea vizuri tu, wasiwasi wetu unatokea wapi?
Abdul Mkeyenge na maneno yangu mengi niliyonayo linapofika suala la mikataba humtanguliza mbele msomi wangu Peter Kadutu. Huyu ndio Jorge Mendes wangu. Akisema nisaini nasaini akisema nisisaini sisaini. Ngasa hongera yako. Mtu mmoja umeweza kuwa Ngasa mahiri ndani ya uwanja na bado ukaenda kuwa Ngasa mahiri nje ya uwanja. Hongera mzee kwa kushinda vita mbili kwa wakati mmoja.
Dunia ya leo ina wachezaji wachache wenye uelewa wa masuala ya mikataba na ubora wa mpira uwanjani. Zamani Chelsea ungewapata Frank Lampard, Juan Mata. Hawa walikuwa na mlinganyo mzuri wa miguu yao uwanjani na mikono yao mezani wakishika peni.
Ronaldo, Messi, licha ya ubora walionao miguuni huwezi kukutana nao mezani kujadili chochote kile. Kuna watu wao maalum wanaosimama nyuma ya kamera. Ngasa amefanya alichokiona sahihi kwake hii mishipa yetu ya shingo inatokea wapi? Si vibaya tukijishangaa badala ya kumshangaa yeye.
Kila mwanadamu amejichagulia aina yake ya maisha. Ngasa amejichagulia kuishi maisha haya anayoishi na ukiona anaendelea kuyaishi fahamu yana masilahi kwake. Huwezi kuishi maisha yasiyo na masilahi. Ikitokea siku ameamua kukacha mkataba wake wa sasa wa Mbeya City baada ya mechi 2 na kwenda klabu nyingine muache tu. Hayo ndio maisha aliyojichagulia.
Binafsi niliwahi kumshangaa katika maamuzi yake mengi, lakini kila nilivyokuwa nikiikumbuka nukuu inayopendwa na Kamwe nilijikuta nabishana na nafsi yangu kwenye kitu kisichowezekana. Ngasa ndio yuko hivi na hajawahi kubadilika. Kama aliweza kuwa mchezaji wa Azam akaenda kushangilia bao na mashabiki wa Yanga waliompa jezi na kuivalia juu jezi inayomlipa mshahara unaanzaje kumshangaa wakati huu alioamua kurejea nyumbani na kuzikacha Free State Stars, Fanja? Tuheshimu uamuzi wake.
Ngasa yuko hivi. Ukimfahamu hakupi shida. El Mereikh ya Sudan waliwahi kumuhitaji kwenye timu yao na kumtaka aende kusaini mkataba na sio kufanyishwa majaribio, viongozi wa timu hiyo walionesha kumuhitaji zaidi na walikuja hadi nchini kumfuata, lakini baada ya Ngasa kujua uwepo wa viongozi hao aliamua kuwazimia simu na kuhama hoteli aliyokuwa akikaa ili kukwepa usumbufu wao. Bado unaendelea kumshangaa Ngasa kwenye maamuzi yake? Kama anajielewa mwenyewe si lazima sisi tumuelewe na tutake afanye tunavyoona sahihi.
Kabla ya wakati huu staa wa timu ya taifa kuwa Mbwana Samatta, mwaka 2009, Ngassa alipata nafasi ya kwenda majaribio nchini Uingereza kwenye klabu ya West Ham. Nafasi hii ilimfanya kila mpenda soka kuamini Ngassa anaenda kushika bendera yetu na kutokomea nayo pale alipoishia Mzee Sunday Manara ‘Computer’ aliyewahi kupiga mpira mwingi katika Ligi ya Uholanzi.
Mawazo ya wapenda soka wa Tanzania yalikuwa tofauti na mawazo ya Ngasa mwenyewe. Katika majaribio yake tulipewa stori nyingi za kumsisimua kila mmoja aliyetega sikio kumsikiliza Shaffih Dauda na kusoma gazeti la Mwanaspoti, lakini mwisho wa yote Ngasa akarejea nyumbani na ujumbe wa kutakiwa aongeze nguvu. Nguvu ni tatizo kwa wachezaji wetu. Lakini tangu Ngasa apewe ujumbe huo hakupitisha miezi sita akaenda zake kuoa. Any way si vibaya alitimiza moja ya nguzo kuu kwenye dini yetu ya Kiislamu.
Tujiulize. Kama Ngasa yule wa 2007 mpaka 2014, alishindwa kupachukia nyumbani na kupapenda nje atakuwa na akili hiyo 2016 muda ambao jina lake linacheza zaidi kuliko yeye mwenyewe? Ngasa alikuwa mahiri. Ubora wake haukuhitaji gari la matangazo mitaani ‘PI’ ili uelezewe. Mashabiki wa soka Kenya walimuita jina la Kisirani kutokana na ubora alionao. Hawakuwa wajinga kumsifu. Unadhani leo wana muda nae tena? Hata ukiwauliza anacheza wapi wakati huu wanaweza wasijue wapi aliko.
Kama Ngasa wa 2009 hakujielewa, Ngasa wa 2016 tunamuelewaje? Karibu nyumbani uncle Ngasa. Si vibaya Mbeya City wakikupa kitambaa cha unahodha uwaongeze vijana wenzio. Lakini ikitokea umeondoka ghafla kama ulivyoamua kuondoka Free State Stars, Fanja, hutatushtua tunajua umezaliwa kuwa hivyo ulivyo kwanini tuanze kupata shida nawe?