Quantcast
Channel: Makala – ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

George Lwandamina na makocha wengine wapya raundi ya pili VPL 2016/17

$
0
0

img_0186

Na Baraka Mbolembole

LIGI Kuu ya kandanda Tanzania Bara (Vodacom Premier League 2016/17) inataraji kuendelea tena wikendi hii. Timu zote 16 zitaanza michezo ya mzunguko wa pili siku za Jumamosi na Jumapili ijayo.

Mwezi mmoja wa dirisha dogo la usajili wa wachezaji linataraji kufungwa siku ya Alhamis (Desemba 15), lakini kingine kinachotaraji kuonekana katika mzunguko wa pili ni maingizo ya makocha wapya katika timu.

GEORGE LWANDAMINA-Yanga SC

Raia huyu wa Zambia alikuwa na mafanikio makubwa katika timu za Zesco United ambayo aliipata taji la ligi kuu Zambia mwaka uliopita (2015) na kuisaidia kufika nusu fainali katika michuano ya Caf Champions League 2016.

Amejiunga na Yanga kuchukua nafasi ya mshindi mara mbili mfululizo wa VPL, Mholland, Hans van der Pluijm ambaye sasa amepandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa ufundi klabuni hapo.

Hans pia aliisaidia Yanga kushinda taji la FA Cup, Mei mwaka huu. Lwandamina ataisimamia Yanga kwa mara ya kwanza katika mchezo rasmi vs JKT Ruvu siku ya Jumamosi katika uwanja wa Uhuru, Dar
es Salaam. Huo utakuwa mchezo wake wa kwanza katika VPL. Je, ataendeleza mafanikio yaliyopita klabuni hapo?

Ameipokea nafasi ya Hans huku timu hiyo ikiwa katika nafasi ya pili ya msimamo na pointi 33 (alama mbili nyuma ya vinara Simba SC). Yanga chini ya Hans ilikuwa ikifunga magoli mengi na kuruhusu machache. Mfano, katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza timu hiyo imefunga magoli 31 na kuruhusu magoli 8 tu.

ABDALLAH MOHAMED-Tanzania Prisons

Baada ya michezo 15 ya mzunguko wa kwanza, Prisons imeachana na kocha Meja Mstaafu, Mingange baada ya kuisaidia kukusanya alama 19. Prisons ilimaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita ikiwa chini ya Salum Mayanga.

Mingange ameondolewa katika timu hiyo ikiwa nafasi ya 7 huku tatizo kubwa kikosini likiwa ni ufungaji wa magoli. Timu hiyo ya Mbeya imefunga magoli 9 tu katika mzunguko wa kwanza hivyo ni kazi kubwa anatakiwa kufanya Abdallah Mohamed ambaye katika mzunguko wa kwanza alikuwa akiinoa Ndanda FC ya Mtwara.

HAMIMU MAWAZO-Ndanda FC

Baada ya kumpoteza kocha Abdallah Mohamed aliyejiunga na Prisons ya Mbeya, Ndanda FC imemrejesha Hamimu Mawazo katika kikosi chao kilicho nafasi ya kumi katika msimamo na alama zao
19.

Hamimu awali alikuwa kocha wa Ndanda kabla ya kuondolewa kumpisha Mingange mwaka uliopita. Ndanda hawako katika nafasi mbaya lakini pointi 19 walizokusanya katika michezo ya mzunguko wa kwanza haziwezi kuwatosheleza kusalia katika VPL.

Hamimu anapaswa kuimarisha safu yake ya ulinzi ambayo imeruhusu magoli 19 kama anataka kufanya vizuri katika timu hiyo.

BAKARI SHIME-JKT Ruvu

Kati ya makocha wazawa wanaofanya vizuri hivi sasa, Bakari Shime ni miongoni mwao. Kocha huyo wa zamani wa JKT Mgambo ya Tanga alikuwa na mafanikio makubwa wakati akiinoa timu ya
Taifa ya Vijana U17 (Serengeti Boys).

Aliiongoza timu hiyo katika michezo 12 pasipo kupoteza. Ametua JKT Ruvu ili kuisaidia timu hiyo
kuondoka chini ya msimamo. JKT Ruvu ipo nafasi ya 14 (nafasi ya mwisho kwa timu tatu zinazoteremka daraja) ikiwa na pointi 13 tu baada ya kucheza 15 ya mzunguko wa kwanza.

Licha ya kuwa na washambuliaji wazuri kama Samwel Kamutu na Atupele Green timu hiyo ya Pwani imefanikiwa kufunga magoli 6 tu huku ikiruhusu nyavu zao mara 12. Kazi kubwa anapaswa kuifanya,
Shime ili timu hiyo isiteremke daraja kwa mara ya kwanza tangu ilipopanda mwaka 2001.

ALLY BUSHIR- Mwadui  FC

Kocha huyu wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania na ile ya Zanzibar amejiunga na Mwadui FC ya
Shinyanga akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ ambaye alijiuzulu mapema katika michezo ya mzunguko wa kwanza.

Bushiri ameichukua Mwadui ikiwa nafasi ya 15 na pointi 13. Mwadui kama ilivyo kwa Prisons, African Lyon, Majimaji FC, JKT Ruvu na Toto Africans nayo inakabiliwa na uhaba wa kufunga magoli huku safu yao ya ulinzi ikiwa imeruhusu magoli 21.

Kumrejesha mlinzi, Malika Ndeule na kumsaini kiungo Awadh Juma kutoka Simba kunaweza kuiinua timu hiyo iliyo na mastaa kama Jerson Tegete, Paul Nonga, Shaaban Kado, Abdallah Seseme, Kabunda, Joram Mvegeke na wengine lakini ukweli, Bushiri amechukua kazi yenye changamoto nyingi sana na atapaswa kuzishinda.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>