Zinedine Zidane alizungumza baada ya mchezo vs Las Palmas kwamba alimbadili Cristiano Ronaldo ili kumpumzisha kuelekea mchezo wa kesho vs Dortmund katika usiku wa mabingwa wa ulaya. Ilikuwa wazi ni kauli ya kisingizio, ukizingatia fomu ya CR7 kwa sasa.
Ronaldo anakikimbiza kivuli chake mwenyewe. Kadri siku zinavyozidi kwenda mbele ndivyo ubora wa Ronaldo unavyopungua na huo ni ukweli usiofichika.
Namba hazidanganyi na kwa upande wa Cristiano – ambaye anapaswa kuangalia takwimu zake mtandaoni kufahamu hali aliyonayo sasa. Mreno huyu amefanikiwa sana kwenye soka kwa sababu namba zake zilikuwa kubwa mno – kuna muda zilikuwa hazina wa kulinganishwa nae. Lakini mpaka kufikia sasa ukiangalia namba zake – zinaonyesha udhaifu mno. Amekuwa na mwanzo mbaya kwenye ligi tangu alipojiunga na Real Madrid.
Hakuna aliyedhani wakati akifunga goli lake la kwanza msimu huu katika mchezo vs Osasuna, ndani ya dakika 10, kwamba hayupo kwenye fomu yake. Angalau kwenye suala la ufungaji kwenye La Liga. Hata hivyo, hilo ndio goli pekee alilofunga msimu huu mpaka sasa kufikia mchezo wa sita. Raundi ya 7 imefika na Ronaldo yupo chini kwenye msimamo wa wafungaji wanaowania Pichichi. Hata, Pedro Leon amefunga magoli mengi kumzidi.
Ronaldo yupo katika msimu wake wa 8 Santiago Bernabeu na inabidi turudi miaka 8 nyuma alipokuwa Manchester United kuona namba ndogo kama za sasa. Msimu wa 2007/09, baada ya michezo 6, alikuwa amefunga goli moja tu. Rekodi yake mbaya zaidi katika La Liga ilikuwa msimu wa 2010/11, alifunga magoli 3 katika mechi 6. Tangu wakati huo hajawahi kufunga chini ya magoli matano katik mechi 6 za kwanza.
Msimu wa 2014-15, aliweka rekodi, alifunga magoli 10 katika mechi 6 za kwanza. Neno ‘slow decline’ linaweza kutumika kama CR7 hatoweza kurudisha kiwango, na tunaweza kushuhudia kile kinachomkumba Wayne Rooney hivi sasa Manchester United.