Na Ayoub Hinjo
Matarajio ya wengi yanaonekana kupishana na uhalisia ambao umeonekana kwa muda mfupi tu ambao ligi imeanza.
Ukimtoa Zlatan Ibrahimovic, Mourinho na Pogba mashabiki wa Manchester United wamewekeza imani kubwa kwa kijana Mfaransa ambaye alitajwa sana na vyombo vya habari vya England wakikosoa dau ambalo alinunuliwa kutoka Monaco.
Mchezo dhidi ya Liverpool ulitosha kuiaminisha dunia miguu yake ilikuwa imebeba maajabu ambayo yaliwafanya mashabiki wa Manchester United kutumia kama kivuli cha kujifichia kutokana na matokeo mabaya yaliyokuwa yanapatikana wakati ule.
Maisha ya Martial sasa yanaonekana kufunikwa na wingu zito ambalo linamtesa na kumfanya ashindwe kutoa alichobarikiwa kwenye miguu yake. Inawezekana Martial anasumbuliwa na arosto ya kutengana na mpenzi wake ambaye sasa anatumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kumchafua Tony ambaye alisaliti kwa kutoka na mpenzi mwingine.
Maisha ya upweke wa Martial yanaonekana kumuelemea na kumfanya ashindwe kwenda sawa na matarajio ya wengi ambao walimtukuza msimu wa jana kwa kiwango maridadi ambacho alikionyesha. Kwa umri wake bado ana mengi ya kuionesha dunia ambayo imempa dhamana kwenye nyasi za uwanjani. Martial anahitaji msaada wa kisaikolojia ili arudi katika ubora wake.
Jose Mourinho ameonekana kutoa nafasi kwa Martial na inaonekana Mourinho bado anaamini miguu ya Hazard imebebwa na Martial ambaye anajitahidi kurejea kwenye nafasi yake. Pia uchovu wa msimu ulioisha unaweza kuathiri kiwango chake cha sasa licha ya kuwa ni mechi chache zimechezwa.
Usajili makini wa Mourinho umefanya utegemezi wa Martial upungue kwenye timu. Macho yapo kwa Ibrahimovic sasa ambaye mipira mingi inaelekezwa kwake. United wanaweza kwenda kushambulia lakini mipira hata mitatu ya ushambuliaji inaweza isipite kwa Martial kama zamani ambapo alikuwa ndio ufunguo wa United msimu ulioisha.
Tony bado ana mengi ya kuonesha ila sasa yupo katikati ya joto na baridi. Yupo katikati ya kufaulu na kufeli. Bado mzunguko wa dunia kwenye muhimili wake unaendelea Martial atarejea tena.