Na Athumani Adam
Natambua safari ya maisha ya soka kwa baadhi ya wachezaji. Mmoja wao ni kiungo wa zamani wa Simba SC mwishoni mwa miaka ya 1990, Marehemu Rajabu Msoma. Marehemu ni kama alijitoa muhanga kipindi kile pale alipoamua kusafiri kilometa nyingi kutoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Kagera.
Hakujali sana miundombinu mibovu iliyokuwepo kipindi kile hususani katika masuala ya usafiri wa barabara, akafanikiwa kujiunga na timu ya RTC Kagera. Baadae akaenda zake Pamba ya Mwanza kabla ya kurudi Dar es Salaam kujiunga na klabu ya wekundu wa Msimbazi Simba SC.
Naikumbuka sana safari hii ya Marehemu Msoma, ilikuwa aambatane na mmoja ya watu wangu wa karibu lakini ilishindikana marehemu alienda peke yake mkoani Kagera. Baada ya kujiunga na Simba Msoma alivutia vijana wengi sana kuupenda mchezo wa soka, alikuwa shujaa kwenye eneo lile.
Kabla ya Msoma, pia sehemu ile ndipo ambapo safari ya fundi wa mpira, Marehemu Methodi Mogella ilianzia bila kumsahau Victor Costa ambaye alielekea Zanzibar kutafuta malisho.
Nimeanza na stori ya Marehemu Rajabu Msoma, baada ya kumsikia Katibu wa chama kimoja cha mpira wa miguu kwenye wilaya moja mkoani Pwani akielezea mpango mkaki wake baada ya kuisha kwa uchaguzi.
Nilishangaa kusikia katibu akikubaliana na Mtangazaji ambaye pia ni mwenyekiti wake kwamba kina Msoma wametoka kisoka kupitia wilaya yake. Katibu alichanganya asili ya mtu na pale alipotokea kisoka. Mfano nani atakubaliana akiambiwa Adam Nditi ametokea kisoka Tanzania?
Hili ndilo tatizo la kuchagua kutokana na asili bila kuangalia watu sahihi ambao wanaishi eneo husika wenye kujua machungu na maumivu ya mpira ya eneo hilo . Lakini Katibu alinishangaza zaidi pale alipokuwa anataja baadhi ya majina ambayo yameingia kwenye kamati mbali mbali za chama hicho.
Nadhani bado asili iliwekwa mbele kuliko kitu kingine chochote. Hivyo ndivyo tulivyo watanzania kwenye mpira siku hizi. Ndio maana ‘Big Boss’ aliamua kwenda kugombea Kagera badala ya Dodoma
Jina la kwanza kwenye kamati ni mchezaji wa zamani ambaye aliwahi kuchezea Majimaji ya Songea. Huyu ana asili ya wilaya ile lakini anaishi Dar es Salaam kwa miaka mingi. Sina shaka na uwelewa wake kwenye soka, lakini umbali kutoka anapoishi sidhani kama anafahamu changamoto za mpira kutoka kwenye wilaya hiyo.
Kila wikiendi yupo pale kwenye uwanja wa taifa unaweza kumkuta mlangoni kama komandoo au kwenye gari anauza tiketi.
Jina la pili, nae ni mchezaji wa zamani wa timu moja kubwa yenye makao makuu katikati ya jiji la Dar es Salaam. Japokuwa ana asili ya wilaya ile lakini maisha yake yapo jijini Dar es Salaam, tena ni kocha wa timu moja ambayo inapatikana katikati ya Uwanja wa Ndege na Tazara.
Nikitazama ukubwa wa wilaya sidhani kama wapo sahihi kuchaguana kutokana na asili. Umbali kutoka Dar es Salaam hadi kuimaliza wilaya hii sio chini ya masaa matatu. Pia bado miundombinu sio mizuri sana hususani wakati wakati wa mvua
Chama hiki cha mkoa ni mfano tu ya kile kinachoendelea kwenye vyama mbali mbali vya wilaya, mikoa na shirikisho. Asili inachukua nafasi kuliko uweledi, kisha wanaojiita watu wa mpira wanajivunia mafanikio ya wachezaji bila kujua mwanzo wake.