Quantcast
Channel: Makala – ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

ARSENAL MSIMU UNAANZA, KUNA KIPI CHA KUTARAJIA?

$
0
0

wp-1471043608364.jpg

Na Richard Leonce

Mimi si mpenzi sana wa usajili wa zimamoto wala usajili wa wachezaji ambao huwa wanakuta tayari ligi imeanza kwa maana ya kwamba wanakua wamekosa maandalizi ya msimu na wenzao. Ndiyo maana kwangu mimi nitauhesabu huu kama msimu wa kwanza kwa Mohamed Elneny pale Arsenal. Ndiyo msimu ambao sasa anaucheza kama mshika bunduki wa kweli.

Ndugu zangu, msimu umeanza. safari mpya ya kushangilia, kuzomea na kuzodoana imeanza tayari na TGM ipo leo kwa ajili ya kutazama kama tunayo matarajio yoyote msimu huu ya kuitetea hata nafasi ya pili tuliyonayo, kwenda juu zaidi kupigania ubingwa au tutarajie anguko kuu.

Nilikua natazama mahojiano ya Arsene Wenger kuelekea kwenye mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili, haonekani kuwa na wasiwasi kama wangu. Na mara nyingine maneno ya mganga huleta nafuu kwa mgonjwa hasa Wenger anaposema anauamini ukuta wake wenye Colum Chambers na Rob Holding.

Huyu Rob Holding hajawahi kucheza ligi kuu tangu azaliwe. Mimi nasubiri kwa hamu kuona huku nikimwombea kwa Mungu afanikiwe kushangaza dunia. Ni kati ya vitu ambavyo hufanywa na Arsene Wenger vya kumpambanisha Holding mwenye thamani ya Pauni Milioni 2 uso kwa uso na Sadio Mane mwenye thamani ya Pauni milioni 34.

Nasubiri kwa hamu sana kuona kwa sababu ni mchezo ambao unaweza ukamalizika kwa Holding kuwa na thamani ya £20 milioni na tukamwita Wenger shujaa lakini ni mchezo ambao unaweza kudhihirisha kauli za siku nyingi kwamba Wenger hana lingine la kutuambia msimu huu.

Ni bahati mbaya sana kwamba tunafungua msimu kwa kukutana na Liverpool ambayo inatajwa kuwa mpya na yenye ari huku sisi tukiamini kwamba Kuna mchezaji atasajiliwa kuja kufunga magoli ili tuzidi kuwa bora. Najua akili za mashabiki wengi wa Arsenal zipo kwenye usajili sasa hivi, wengi wakimuwaza walau beki Shkordan Mustafi. Wanasahau hata kama watamsajili, bado hatowasaidia kwenye mchezo wa ufunguzi wala michezo michache ijayo.

Najaribu kuivuta lakini siipati picha ya hali itakavyokua kama tutapoteza mchezo dhidi ya Liverpool.
Ni mchezo wa kawaida ambao hauwezi kukupa tafsiri ya haraka ya kampeni yako kama unashinda, lakini ni mchezo ambao utavuruga kabisa hewa kama Arsenal watapoteza, na pengine itamlazimu Wenger kukimbia haraka sokoni kufanya kitu ambacho kwa lugha ya mpira tunaita ‘panic buy’. Mungu aepushie mbali.

Tukirudi kwenye kikosi, pale nyuma hakuna jinsi ambavyo Wenger anaepuka kusajili beki mzoefu. Nafurahi kusikia anamtaka Mustafi. Kama atampata atakua amebaki na kazi moja tu ya kusajili mshambuliaji.

Timu inahitaji beki hata kama Gabriel ambaye atakosa wiki kama 7 au 8 na Per Mertesacker ambaye hatutamuona uwanjani mpaka mwakani wangekuwepo. Bado Arsenal ilihitaji beki mwingine mzuri lakini hitaji linaongezeka sasa hivi wakati Laurent Koscielny akiwa hayupo tayari kucheza, lakini hata akiwa tayari anakuwa ndiye beki pekee mzoefu kikosini na hatujui ya kesho, baada ya mchezo wa Liverpool si ajabu tukapokea majeruhi wengine.

Bado namuona Hector Bellerin kama mtu anaehitaji kukua zaidi, sina wasiwasi nae lakini nina machozi kwa mbali kwa Kieran Gibbs. Bado naamini ana kitu cha kutuonesha kama beki wa kushoto lakini ana kazi ngumu ya kumwondoa Nacho Monreal mahali alipo. Nafurahi hakuna habari ya Gibbs kwenda mahali hata kwa mkopo.

Kama kuna eneo halihitaji kuguswa kwa sasa basi ni eneo la katikati. Baada ya kumpigia kelele nyingi sana Arsene Wenger hatimaye amekubali kufanya kilekile tulichokisema japo amechelewa sana, labda alisubiri akina Flamini na Arteta waondoke lakini kuwaongeza Elneny na Granit Xhaka kikosini, hapa Wenger amefuta kabisa ule wasiwasi uliokua unatanda pindi Francis Coquellin alipokua anakosekana.

Kama kuna maumivu ya kichwa duniani basi ni ya kuwapanga akina Ramsey, Özil, Cazorla, Xhaka, Elneny, Coquellin na Wilshere ili wakuundie safu ya kiungo. Maumivu yako yatatokana na yupi umwache nje kwa sababu gani kama wote wapo fit. Lakini katika ulimwengu wetu wanaarsenal tunajua ni jinsi gani huwa tunateswa na majeruhi, hivyo kuwa na machaguo mengi namna hii ni faraja kubwa.

Tunakwenda kwenye msimu mpya nikiwatazama kwa jicho la tatu la upendo vijana ambao naamini wanakwenda kuunda kizazi kipya cha Arsenal. Umepata muda wa kuwafikiria japo kidogo Joel Campbel, Alex-Oxlade Chamberlain na Alex Iwobi?
Kama Mungu atawapa afya hawa vijana, natarajia maisha magumu kidogo kwa Theo Walcott.

Tatizo kubwa ambalo naliona lipo kwenye safu ya ushambuliaji. Huwa tunatofautiana sana maoni juu ya Olivier Giroud, mimi binafsi nampenda sana, ni mshambuliaji mzuri lakini siyo kweli kwamba anaweza kukupa Ubingwa bila usaidizi.

Nilikua napiga hesabu nikakuta msimu mzima uliopita, Olie alifunga jumla ya mabao 31 kwa maana ya klabu na timu ya taifa ya Ufaransa. Yangeweza kuwa mengi zaidi lakini tunajua kwamba aliteswa na majeraha kwa muda. Lakini bado 31 siyo magoli machache kiasi cha kusema mshambuliaji huyu hafai.

Lakini ni Giroud huyu huyu kwenye msimu huo huo alicheza mechi 22 akafunga magoli mawili tu. Hii inakufunza kwamba kama una mtu mbadala ambaye si majeruhi wa miezi tisa kama Danny Welbeck angeweza kukusaidia wakati Olie akitafuta yalipo magoli yake. Mara nyingine magoli hukauka, huwa yanawakauka hata akina Christiano Ronaldo.

Bahati mbaya sioni mshambuliaji sokoni ninayemtamani ambaye anaweza kuja kumfanya Giroud awe chaguo la pili, lakini si salama kwenda kwenye msimu huu bila kuongeza mshambuliaji. Tusijidanganye kwamba Alexis Sanchez anaweza kucheza kama mshambuliaji wa mwisho, ndiyo anaweza lakini kwa michezo michache sana.

Sanchez alicheza kama mshambuliaji wakati fulani mwaka 2013/14 akiwa Barcelona na akafunga mabao 19 tu. Hiyo ni idadi ambayo anaweza akafunga hata akitokea pembeni. Lakini pia usitarajie Sanchez anaweza kuwa mtulivu wa kusubiri mipira pale mbele, Sanchez anapenda kuuchezea mpira na kumpanga kama mshambuliaji ni kumnyima haki yake.

Arsene Wenger ameanza dalili za kumfanyia hivyo Sanchez na wengi wanamsifu lakini mimi sioni kama hiyo ni tiba ya matatizo ya Arsenal kwenye eneo hilo. Wenger anapaswa kusajili mtu hapa. Nimeambiwa yule Asano Takuma bado anapaswa kucheza kwa mkopo huko kwao kwa msimu mzima ndiyo atapata Visa ya kufanya kazi nje ya Japan kwa hiyo ni lazima Wenger afanye la kufanya kama ni kweli amedhamiria kitu msimu huu.

Nawatakia msimu mzuri washika bunduki wenzangu, hatuna kikosi cha ubingwa lakini pia hatuna kikosi kibovu. Tutaufurahia msimu na usiache kushare na mimi chochote kinachotuhusu kupitia twitter ya @chardboy77 au 0766399341.

 


Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>