Na Baraka Mbolembole
Katika dunia ya sasa kufanikiwa katika jambo lolote ni lazima kuwe na maandalizi ya kweli katika jambo husika.
Lakini katika karne hii ya 21 jambo moja zaidi linalo changia kutofanikiwa kwa mambo mbalimbali ni kwamba ‘mamlaka ya kuamua yapo mikononi mwa watu wachache sana,’ na watu wenye mamlaka hayo wanashindwa kutambua kuwa miaka mia moja nyuma kiasi kidogo tu fedha kingetosha kujenga uwanja wa michezo, tena mkubwa zaidi ya huu wa sasa (uwanja wa taifa)
Lakini kwa utaalamu wa sasa hakuna uwezekano wa kujenga hata hostel ya timu, sababu ya fikra mgando, ubinafsi uliopitiliza, falsafa za zamani kwa waliopewa majukumu ya kuutoa mpira wetu katika shimo tulilopo.
Kwa mfano, Henry Ford ‘mtaalamu wa zamani’ katika utengenezaji wa magari. Alianza kazi ya kutengeneza magari katika kiwanda kidogo cha kutengenezea baiskeli, akajenga uwezo wake polepole, lakini katika miaka hii, mtu yeyote anayeamua kuanzisha kiwanda cha kutengenezea magari ni lazima ajiandae kutumia kiasi kikubwa cha pesa kabla gari la kwanza halijatoka na kuanza kutembea barabarani.
Henry alikusanya mawazo yake na kuangalia namna ya kuyafanyia kazi, wala hakuamini katika njia ya mkato kama viongozi mbalimbali wa katika nchi yetu.
Kwa nini ulianza kuangalia mpira kwa mara ya kwanza?
Baadhi ya wanachama wa Yanga SC wanafurahia, lakini wadau na mashabiki wa kandanda nchini wapo katika mshangao! Lakini ndiyo hivyo tena, inawezekana siku ya Jumanne klabu hiyo ya kwanza kuanzishwa nchini Tanzania (1935) ikaweka historia ya kuwa klabu ya kwanza barani Afrika na pengine duniani ‘kukodishwa.’
Uamuzi wa kuikodisha klabu hiyo kwa miaka kumi kwa tajiri na mwenyekiti wa sasa wa klabu, Yusuf Manji umefikiwa katika mkutano wa dharura siku ya Jumamosi ya August 6. Si kuuzwa, kama inavyozoeleka bali kukodishwa.
Inashangaza sana, lakini upande wangu ‘nimeupenda mpango huo’ kwa maana umedhihirisha ni kwa kiasi gani wanachama wa klabu hiyo wasivyo na hoja. Ni waoga! Si wadadisi, na pengine wana hofu ya ‘maisha bila Manji.’
Hii ndiyo Tanzania, nchi ambayo watu masikini wapo tayari kuongozwa hata kinyume na katiba ikiwa tu ‘mtawala’ atakuwa ni ‘mtu tajiri.’ Wanachama wa Yanga ndiyo walimuomba, Manji kuongoza klabu yao hata kwa miaka kumi zaidi mwaka 2014. Labda kama imesahaulika.
Si hivyo tu, wengine walimpigia magoti huku wakitoa machozi ya kilio, wakimuomba Manji kutoiacha klabu yao. Wakamuomba awe kiongozi bila kufanyika kwa uchaguzi. Walivunja katiba yao wenyewe na nakumbuka wakati ule niliandika makala katika mtandao wa shaffihdauda.co.tz iliyokuwa na kichwa cha habari, ‘WANACHAMA YANGA SC, BAADA YA UAMUZI NI UTII…’
Manji alikuwa amemaliza muda wake wa uongozi ( 2014) na hakuwa na mpango wa kuendelea kuongoza timu hiyo.
Mambo mawili katika demokrasia, ukiyakosa mambo hayo basi tambua hakuna demokrasia. Kwanza, kila mwanachama alipaswa kusema kwa uhuru, na maneno ya kila mtu yanapaswa kusikilizwa, hata kama mawazo yake hayapendwi kiasi gani.
Kama mtu anapendwa kwa wema wake, au hapendwi kwa visa vyake, hayo yote si kitu. Kila mwanachama wa Yanga, lazima aweze kusema kwa uhuru. Watu wenye mawazo tofauti hata wakiwa wachache, ni lazima wawe na haki ya kutoa mawazo yao katika mkutanomkuu wa klabu bila hofu ya kusumbuliwa.
Mawazo yao yashindwe katika hoja za majadiliano. Majadiliano yenyewe yatakayoleta uamuzi lazima watu wawape nafasi ya kusema kwa uhuru, na hata baada ya kuamua jambo wanachama wawe na uhuru wa kuendelea kulizungumza jambo hilo.
Wale wachache wenye mawazo tofauti lazima wafahamu kuwa kama wanayo mawazo yenye maana, na kama wakiyaeleza mawazo hayo vizuri. Wanaweza kubadili mawazo ya wale walio wengi.
Lakini, Manji amekuwa ‘dikteta’ na nimesikitishwa sana na uamuzi wake wa kuwafuta uanachama baadhi ya wanachama tena bila hata kupewa nafasi ya kujitetea kwa kuwa tu ni ‘watu wadadishi, wenye hoja ya mitazamo mingine tofauti na ile ya kwake.
Ndiyo, aliwauliza wanachama wake mara tatu, iwapo awavue uanachama wa klabu au la! Na hakuna mwanachama ye yote katika ukumbi ule wa mkutano aliyesema, ‘HAPANA!,’ wote walisema ‘Ndiyo.’
Tunaondoa kirahisi sana katika mpira, mtu unalazishwa kuichukia timu uipendayo kwa sababu ya hoja tu! Hoja nzito ambayo kiongozi mwenye mamlaka haitaki.
Niwashauri tu wale wanachama wa Yanga walio nje ya Dar es Salaam, ni ‘ujinga’ kulisumbua Jeshi la Polisi. Nasikia wamekuwa wakihamasishana kufanya maandamano ya nchi nzima kupinga uamuzi wa klabu kukodishwa kwa miaka kumi-timu na Logo huku wao wakibaki na majengo pekee!
Sasa wanataka kwenda kupinga nini wakati uamuzi umetolewa na wanachama wote waliokuwapo katika mkutano wa klabu? Kama uamuzi umepitishwa katika mkutano wa wanachama, ambaye hakuwapo ‘imekula kwake.’
Ni vyema wajipange tu kuendelea kuisapoti timu yao kwa miaka kumi ijayo ndani ya uwanja, huku wakisubiri asilimia 25 ya faida ambayo Manji ataipata katika uwekezaji wake. Wapo ambao wamekuwa wakihoji, Yanga itapata faida gani kwa kumuachia Manji timu na logo?
Faida itakuwapo tena kubwa tu kuliko klabu kubaki hivi ilivyo sasa. Swali la msingi, Yanga inakodishwa kutoka katika katiba/kanuni zipi?
Narudia tena kusema; ‘ Mtu mkubwa ni Mwanafunzi.’ na maana halisi ya neno falsafa ni ‘ Kutafuta busara, kupenda hekima’. Falsafa linatokana na maneno mawili ya Kiyunani; ‘ Philo’ lenye maana ya ‘ Upendo juu ya jambo fulani’ na ‘ sophia’ lenye maanaya ‘ busara’.
Wakati anaingia Yanga kama mwenyekiti katikati ya mwaka 2012, Manji alikuwa mtu mgeni kabisa katika tawala za soka na miaka yake minne amefanikisha mataji matatu ya ligi kuu na moja la FA, kimataifa pia amefanikiwa sana. Timu ipo 8 bora Caf Confederation Cup 2016.
Haya ni mafanikio kwa kiongozi yeyote. Lakini naye tayari ameshafahamu udhaifu mkubwa wa kimawazo walio nao wanachama wake. Yaani, hata Kifukwe ameshindwa kuhoji ni kwanini timu inakodishwa!
Wanachama wa Yanga siwalaumu kwa maamuzi yenu, ila mbona miaka miwili hii mmekuwa watu wa ‘ndiyo, ndiyo tu, nyie hamuwezi kusema, hapana?
Baada ya kusainiwa kwa kandarasi ya ukodishwaji wa klabu hiyo nitakwambia ni kwanini Yanga ‘itatusua’ ila timu inakodishwa kutoka katika taratibu gani kikatiba? Hili ndiyo swali la kujiuliza.
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu #BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.