Quantcast
Channel: Makala – ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

NIONAVYO MIMI: MO APEWE SIMBA LAKINI SIYO KWA 51% – 2

$
0
0

IMG_0392

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii, nilianza kwa kumjadili Mo na historia yake ndani ya Simba. Nilienda mbali nakukumbushia kidogo kilichokuwa kikitokea zamani enzi za wafadhili. Kwa kifupi, nilizungumzia faida ambazo Simba inaweza kuzipata chini ya Mo.

Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho, nitajikita zaidi kwenye  kuzungumzia upande wa pili wa ‘dili’ la kuuza hisa za 51%, ambao kimsingi ndiyo umebeba makala hii.

Kuuza hisa kwa 51% ndiyo sakata lililomfanya Mzee Yusuph Mzimba awe shujaa wa Jangwani wakati Francis Kifukwe na Abbas Tarimba walikuwa wakipigia chapuo wazo ka kuigeuza Yanga kuwa kampuni.

Hoja ya Mzimba ilikuwa hivi, huwezi kuanzisha kampuni ndani ya klabu halafu hiyo kampuni ikawa kubwa kuliko klabu. Katika masoko ya hisa na mitaji, mwenye hisa nyingi ndiyo mwenye sauti kwa hiyo endapo klabu itakuwa na hisa chache( 49%) maana yake haitakuwa na sauti kwenye maamuzi.

Madhara ya kukosa sauti ni kushindwa kupinga baadhi ya mambo ambayo klabu (wanachama) wanaona hayaendi sawa.

Unaweza ukaiangalia Simba chini ya mikono ya Mo, ukaiona iko salama…lakini swali rahisi ni, je Mo atakaa na Simba maisha yote? Hawezi kuja kuiuza kwa wawekezaji wengine wenye mapesa zaidi yake?

Kutokana na mpira kuwa bidhaa yenye mvuto mkubwa duniani, wafanyabiashara wengi wamevutiwa kuwekeza na kushuhudia klabu nyingi zikiangukia kwenye mikono ya matajiri ambao wengi wao huangalia faida ya kibiashara tu bila kujali maendeleo ya mchezo wenyewe.

Kwenye hili, nitatoa mfano wa timu moja ya England, Portsmouth maarufu kama Pompey, ambayo ‘mashabiki wa soka waliozaliwa wakati Jakaya yuko madarakani’, wanaweza wakawa hawajawahi kuisikia kabisa, achilia mbali kuiona zikicheza.

Portsmouth ni mabingwa wa Kombe la FA mwaka 2008, wakiifunga Manchester United kwenye nusu fainali tena machinjioni Old Trafford. Kumbuka 2008 United walikuwa mabingwa wa England na Ulaya. Lakini kwa sasa, Pompey,  wanacheza league two ambayo ni sawa na daraja la nne.

Mwaka 2006, Pompey waliangukia kwenye mikono ya mfanyabiashara tajiri Alexandre ‘Sacha’ Gaymak ambaye alitaka kuifanya Portsmouth itawale soka  la England ghafla bin-vuu. Alikopa mapesa mengi kutoka mabenki mbalimbali na kununua wachezaji wapya takribani kikosi kizima katikati ya msimu.

Uwekezaji wake ukalipa mwaka 2008 walipotwaa kombe la FA lakini hata hivyo, mzigo wa deni ukawa mkubwa na kuanza kuitafuna klabu.

Mwaka 2009, Gaydamak akaiuza klabu hiyo kwa mfanyabiashara kutoka Saudi Arabia, Sulaiman Al Fahim ambaye alianza kwa kuwaondoa wachezaji wote waliokuwa wakilipwa mishahara mikubwa. Glen Johnson akauzwa Liverpool, Peter Crouch na Niko Kranjcar wakauzwa Spurs na Sylvain Distin akatimkia Everton.

Lengo lilikuwa kubana bajeti lakini hata hivyo, hali iliendelea kuwa ngumu na klabu ikashindwa kuwalipa mishahara wachezaji waliobaki.

Al Fahim akaiuza klabu kwa Ali Al Faraj, raia mwingine wa Saudi Arabia ambaye alikuwa hajawahi hata kuingia uwanjani kuiona Pompey ikicheza.

Wakati mzigo wa madeni ukiendelea kuibana klabu hiyo, mmiliki mpya akaenda kukopa tena pauni milioni 17 kutoka kwa tajiri mwingine Balram Chainrai

Kutokana na madeni, klabu ikazuiliwa na ‘bodi ya ligi’ kufanya usajili mpya mpaka ilipe madeni yake ya usajili kutoka kwa Chelsea na Arsenal kutokana na kuwasajili Glen Johnson na Lassana Diarra mtawalia.

Ili kukabikiana na hilo, ikabidi wachezaji wengine muhimu, Younous Kaboul na Asmir Begovic wauzwe na pesa zikatwe na ‘Premier League’ (bodi ya ligi) kulipa deni hilo.

Mlolongo wa madeni na msururu wa wamiliki uliendea mpaka mwaka 2013, mashabiki kupitia chama chao cha Portsmouth Supporters Trust walipochangishana na kuinunua klabu yao.

Klabu hiyo kwa sasa ipo chini ya umiliki wa wanachama na hawataki tena kusikia habari za wawekezaji.

Mikasa kama hii ni mingi na imezitafuna klabu nyingine kadhaa kama Leeds United, mabingwa wa England 1992 na wananusu fainali wa ligi ya mabingwa Ulaya 2002.

Miaka ya 90 na 2000 mwanzoni, ulikuwa ukizungumzia ‘Top Four’, ulikuwa unawazungumzia Leeds, Aston Villa na wengine, leo hii hawa jamaa hawapo kutokana na hii 51%.

Uwanja wa Stamford Bridge unaotumiwa na Chelsea, unamilikiwa na mashabiki wa timu hiyo ambao pia wana miliki haki ya jina la klabu hiyo. Sababu ni kwamba, huu mpango wa 51%, kuna wakati uliangukia kwa watu wenye maamuzi ya hovyo, wakakopa mapesa mengi na klabu ikashindwa kulipa. Wakauza uwanja kwa makampuni ya waendeleza milki ambayo yakataka kubadilisha matumizi na kujenga majumba ya kupangisha.

Mashabiki wakapambana na kampuni hiyo mahakamani mpaka wakashinda. Wakailipa pesa zake na mpaka sasa uwanja ni wao. Ili kuwadhibiti wamiliki wajao, mashabiki hao wakaweka kipengele kwenye mkataba na klabu juu ya kuutumia uwanja huo kwamba ikihama uwanja basi ibadilishe na jina.

Mo ana nia nzuri na Simba na yeye ni shabiki wa Simba, lakini ikumbukwe kwamba hata Mike Ashley ni shabiki wa Newcastle lakini maamuzi yake mara zote yanawaumiza mashabiki wenzake na kila mwaka wanalala mapema….mwaka huu ndiyo wameshuka daraja kabisa.

Endapo klabu hizo nilizozitolea mfano hapo juu, zisingekuwa na kautaratibu ka 51%, bila shaka mashabiki wangepinga baadhi ya maamuzi na leo hii Pompey wasingefilisika, Leeds na Aston Villa wangekuwa top four na Stamford Bridge ingekuwa unamilikiwa na Chelsea yenyewe.

Zaka Zakazi

0718171078


Viewing all articles
Browse latest Browse all 676

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>