Kiungo wa Manchester United Bastian Schweinsteiger ametangaza rasmi kustaafu soka la kimataifa baada ya kucheza michezo 120 kwa taifa lake la Ujerumani.
Schweinsteiger (31) ni moja ya wachezaji waliocheza mechi nyingi zaidi kwa taifa lake, huku akiwa amecheza michezo mitano tu kwenye Euro mwaka huu na kufanikiwa kufika mpaka nusu fainali, ambapo walitolewa na Ufaransa.
Schweinsteiger, ambaye kwa mara kwanza kabisa alicheza Ujerumani mwaka 2004, amefanikiwa kuwemo kwenye kikosi kilichoshinda Kombe la Dunia mwaka 2014 baada ya kuifunga Argentina, baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu mwaka 2006 na mwaka 2010. Vile vile ana medali a shaba aliyopata kwenye michuano ya Euro mwaka 2008.
“Muda si mrefu, nimemwomba kocha asinijumuishe tena kwenye kikosi cha timu ya taifa kwenye siku zijazo, kwasababu ninataka kustaafu,” aliandika
“Nimefanikiwa kucheza michezo 120 kwa taifa langu na nimepata wasaa mzuri sana ambao hakika nashindwa hata jinsi ya kuelezea na kwa maana ya uzuri na mafanikio pia.”
“Jogi Low alijiua namna gani ya Michuano ya Euro mwaka huu iliyofanyika nchini Ufaransa ilivyokuwa na maana kwangu kwasababu kiukweli nilitaka kushinda taji ambalo hatujaweza kulipa tangu tulivyofanya hivyo mwaka 1996.
“Lakini ndiyo hivyo tena haikuwa bahati yangu, lazima nikubaliane na hali halisi.
“Kushinda Kombe la Dunia mwaka 2014 ilikuwa ni jambo la kihistoria ya aina yake ambayo kikukweli siwezi hata kuelezea.
“Na ndiyo maana ni sahihi na inaleta maana kuchukua maamuzi haya na kuitakia timu mafanikio mema katika harakati za kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018.
“Nimeamua kuchukua maamuzi ya kuacha kuitumikia timu ya taifa ambayo imekuwa familia bora sana kwangu. Natumaini kwamba mahusiano yangu hayatavunjika bali yatabaki kuwa imara kwa namna moja ama nyingine.
“Mimi ningependa tu kuwaambia mashabiki wetu: ‘ilikuwa ni heshima kubwa sana kucheza kwaajili yenu ninyi. Shukrani nyingi sana nielekeze kwenu na asanteni sana kwa kila kitu ambacho tulifanya bega kwa bega.”